MADRID, Hispania
KATIKA Ligi Kuu Hispania maarufu kama La Liga,
Barcelona ndiyo timu pekee inayoonekana kuwa na rekodi ya asilimia 100 kwa
msimu huu.
Barcelona ndiyo mabingwa watetezi wa La Liga, wana
rekodi asilimia 100 baada ya kushinda mechi zao zote tatu za kwanza za ligi.
Mabosi wengine wa ligi hiyo, Real Madrid wana rekodi
ya asilimia 85 kwa kuwa mechi moja walitoka sare. Sasa wanashika nafasi ya pili
nyuma ya Barcelona iliyokusanya pointi 9 katika mechi hizo tatu.
Madrid ndiyo inaanza kushuka dimbani leo, ikiwa
nyumbani itakipiga dhidi ya Granada, timu ambayo kwa rekodi inaonekana huwa haiwasumbui,
wakikutana nayo katika mechi za mwanzoni.
Granada wamekuwa ‘wabaya’ kila wanapokutana na Real
Madrid katika mechi za mwishoni mwa ligi, kwani wamekuwa wanachelewesha au hata
kuwakosesha kutwaa ubingwa.
Barcelona wakiwa na uhakika wa hiyo asilimia 100 ya
ushindi katika mechi zao tatu, nao watashuka dimbani kesho dhidi ya Levante
ambayo katika msimamo wa ligi iko katika nafasi ya 15.
Mechi iliyopita kwa Barcelona ilikuwa ngumu, lakini
wakaitandika Atletico Madrid kwa mabao 2-1, Lionel Messi alifunga na kufikisha
mabao 286 ya La Liga. Sasa wanaweza kuwa na nafasi nzuri ya kuendeleza rekodi
nzuri ya ushindi ya mechi yake ya nne.
Kingine kinachovutia katika ushindani wa timu hizo
mbili ni namna watumishi wao tegemeo walivyo. Messi kwa upande wa Barcelona
akiwa na Neymar na Luis Suarez wanaonekana wako vizuri tu.
Cristiano Ronaldo anaonekana kuwa gumzo zaidi kwa
kipindi hiki na anatupiwa macho na wengi. Ndani ya mechi mbili amefunga mabao
manane.
Mechi moja ya La Liga dhidi ya Espanyol na nyingine ya
Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Shaktar. Hiyo imeamsha morali ya Madrid chini
ya kocha mpya Rafa Benitez.
Hauwezi kukwepa ushindani wa Ronaldo na Messi kwa kuwa
umekuwa ukizidi kuleta raha ndani ya La Liga lakini hadi nje unapozungumzia
Bara la Ulaya au Tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia.
Wawili hao, kila mmoja ana aina yake ya uchezaji
lakini kila mmoja ana mafanikio na mashabiki wake ambao wanaridhika na utendaji
wake.
Ronaldo ataendelea kutupia lundo la mabao kama
alivyofanya katika mechi mbili zilizopita? Messi naye atasimama na kujibu
mashambulizi? Ni suala la kutulia katika runinga yako na kuangalia kwa raha.
Watanzania kwa kipindi hiki wamekuwa na bahati zaidi
kwani Azam TV watakuwa wakionyesha mechi za La Liga moja kwa moja.
Kuonyeshwa kwa mechi hizo, tena kwa kiwango cha malipo
nafuu ya ving’amuzi, kunawapa nafasi Watanzania hao kujua vizuri ubora wa La
Liga.
Kitakwimu, La Liga ndiyo ligi kubwa zaidi duniani.
Hivyo ni nafasi nyingine kwa wapenda soka nchini kupima kuhusiana na hizo
takwimu na ubora wa La Liga badala ya kuhadithiwa kama ilivyokuwa awali.
LEO JUMAMOSI:
Real Madrid Vs
Granada
Valencia Vs
Real Betis
Eibar Vs Atletico
Madrid
Real Sociedad Vs Espanyol
KESHO JUMAPILI:
Sevilla Vs
Celta Vigo
Deportivo Vs Sporting Gijon
Villarreal Vs Athletic
Bilbao
Barcelona Vs Levante
Las Palmas Vs Rayo Vallecano
0 COMMENTS:
Post a Comment