Ile rekodi iliyodumu kwa takriban siku zisizopungua 103 ya timu ya
Azam kucheza mechi za kimashindano bila ya kuruhusu kufungwa bao ndani ya
dakika tisini, hatimaye imevunjwa rasmi mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mara ya mwisho Azam kufungwa bao katika mechi za kimashindano
ilikuwa Mei 6, mwaka huu walipovaana na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar,
lakini baada ya hapo hawakuruhusu tena bao lolote.
Kiungo mshambuliaji wa Yanga raia wa Brazil, Andrey Coutinho ndiye
aliyekuwa mchezaji wa mwisho kuifunga Azam kwa bao lake pekee wakati Yanga
ikifungwa 2-1 na timu hiyo.
Coutinho alifunga bao hilo katika mchezo muhimu kwa Azam kutokana
na siku hiyo mabingwa hao wa Kombe la Kagame, Azam kuhitaji ushindi utakaoipa
nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa na wakafanikiwa.
Lakini baada ya kupita kipindi hicho chote, Jeremiah Juma wa
Tanzania Prisons akaja kuivunja rekodi hiyo kutokana na kufunga bao moja
walipokubali kipigo cha mabao 2-1 katika Uwanja wa Azam Complex ukiwa ni mchezo
wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu, Jumamosi iliyopita.
Ikumbukwe kuwa, tangu mara ya mwisho Azam iruhusu bao langoni mwao
na kabla ya mchezo wa wikiendi iliyopita, imefanikiwa kucheza mechi nane za
kimashindano, ukiacha zile za kirafiki, moja ya ligi, nyingine ya Ngao ya Jamii
huku zingine sita zikiwa ni za Kombe la Kagame na ikifunga mabao 11.
0 COMMENTS:
Post a Comment