Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Kocha Mkuu wa Stand United ya
mkoani hapa, Mfaransa, Patrick Liewig, amenusurika kupigwa na mashabiki wa timu
hiyo kutokana na timu yao kufungwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar, hivyo kujaa hasira
na kutaka kumvamia kwenye vyumba vya
kubadilishia nguo.
Baada ya mchezo huo kwenye Uwanja wa Kambarage, mashabiki wa Stand
waliokuwa jukwaani, walishuka kwa wingi na kutaka kuingia kwenye vyumba vya
kubadilishia nguo, lakini wakazuiwa na askari polisi waliokuwepo uwanjani hapo.
Mashabiki hao walibainisha kuwa kocha wa timu yao hana uwezo wa kuipatia
ushindi timu hiyo kwani amekuwa akiwakoromea wachezaji na kuwatoa mchezoni,
jambo ambalo kwa kocha wa kawaida hawezi kulifanya.
“Sisi tulipanga tumpige
kutokana na kushindwa kuiongoza timu yetu kupata ushindi, halafu huyu kocha
hana uwezo wa kufundisha timu zaidi ya kulalamika kila wakati na kuwatoa
wachezaji mchezoni,” alisema kwa hasira mmoja wa mashabiki hao.
Mashabiki hao walilalamika kuwa, haiwezekani mchezaji mzuri kama
Haruna Chanongo awekwe benchi halafu achezeshwe Amri Kiemba ambaye uwezo wake
ulionekana wa kawaida sana.
Mashabiki hao walisikika wakipiga kelele kuwa hawamtaki Liewig,
aliyewahi kuifundisha pia Simba, badala yake wanamtaka Mganda, Mathias Lule
ambaye aliifundisha timu hiyo msimu uliopita, awe kocha mkuu wa timu hiyo,
kwani ameshaizoea na anaweza kuibadilisha.
Bao la dakika ya 90 la Rogers Freddy, ndilo lililozima kelele zote
za shangwe za Stand.
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, Championi Jumatatu
lilishuhudia Liewig akiwafokea hadi makocha wenzake kwenye benchi lake la
ufundi.
0 COMMENTS:
Post a Comment