LIGI Kuu Bara imeanza katika mechi nane za juzi na jana,
kila timu kati ya 16 zinazoshiriki ligi hiyo imeshuka dimbani na inajua imevuna
nini.
Takwimu zinaonyesha hivi, katika mechi nane za timu hizo
16, mabao 12 yamefungwa huku timu 7 zikishinda katika michezo saba kasoro mmoja
tu ambao ulikuwa una matokeo ya sare.
Mechi hizo zilikuwa hivi, African Sports ililala kwa bao
1-0 ikiwa nyumbani dhidi ya Simba, Majimaji ikashinda nyumbani kwa bao 1-0
dhidi ya JKT Ruvu huku Azam FC ikiiangusha Prisons kwa mabao 2-1.
Stand United ikiwa nyumbani ikalala 1-0 dhidi ya Mtibwa
Sugar, Mwadui wakasafiri hadi jijini Mwanza walikoambulia kipigo cha bao 1-0
kutoka kwa Toto African huku Mbeya City wakilala nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya
wageni wao Kagera Sugar.
Yanga ambao ni mabingwa watetezi, ndiyo wamefunga pazia
la mechi za ufunguzi baada ya kucheza mechi ya nane dhidi ya Coastal Union
kwenye Uwanja wa Taifa na kuigaragaza kwa ushindi wa mabao 2-0 ambao ndiyo
mkubwa zaidi katika mechi hizo za ufunguzi.
Takwimu zinaonyesha timu tatu zimeshinda zikiwa ugenini
huku nne zikishinda nyumbani na mechi pekee ambayo imekuwa na sare ni ile kati
ya Ndanda FC iliyokuwa nyumbani dhidi ya Mgambo Shooting.
Unaweza kusema ligi imeanza ikiwa na picha tofauti
kabisa ingawa picha yenyewe inaonyesha wazi kwamba imeganda upande mmoja na
kutakuwa na ushindani mkali na zaidi ni kwa walewale vigogo.
Yanga, Simba na Azam FC ambao kila mmoja amebeba pointi
tatu, watabaki kileleni kwa kuwa mwanzo hawakuonyesha mchezo mzuri sana huenda
kwa kuwa ligi ndiyo inaanza lakini wameibuka na pointi tatu.
Ushindani wao kwa kuonyesha kweli wana vikosi ambavyo
vitaenda vinaimarika na wachezaji kuzoeana zaidi hivyo kuamsha ushindani zaidi.
Kuna kitu ambacho kimejionyesha, mechi nane za kwanza za
ligi. Timu tatu zimeshinda ugenini na moja imepata sare kwa kukataa kufungwa.
Hii inaonyesha pia mechi hazitakuwa rahisi, kwamba
hakuna urahisi kwa timu kwa kuwa tu inacheza nyumbani badala yake inatakiwa
kujituma.
Bado inaonyesha timu ambazo hazina wachezaji wenye
majina makubwa sana, wanaweza wakatoa ushindani pia na kuwapa wakati mgumu
ambao wanaaminika.
Angalia Mwadui FC inayoundwa na wachezaji wengi makinda,
wameweza kuigaragaza Mwadui FC yenye wachezaji wengi magwiji na wazoefu kama
Athumani Iddi ‘Chuji’, Nizar Khalfan, Shabani Kado na wengine wengi.
Mbeya City ikalala nyumbani, lakini bado katika timu nne
zilizopanda daraja, mbili zikashinda na mbili zikapoteza. Hivyo, inaonyesha
kutakuwa na ushindani kutoka kwa timu hizo zilizopanda na hazitakubali kirahisi
kurejea daraja la kwanza.
Ukiangalia kiwango cha waamuzi, unaweza walijitahidi kwa
kiasi kikubwa kutokana na kiwango tulichokizoea.
Huenda utakuwa ni wakati mwafaka wa wao kuwa walinzi wa ubora
wa ligi hiyo kwa kuchezesha kwa haki na kufuata hasa sheria 17 ili kuepusha
kuzusha figisu na kusababisha kuyumba kwa kilichoanza kuonekana.
Asilimia kubwa ya timu zimeonyesha ushindani lakini
mategemeo ni ushindani zaidi ya huo. Kawaida timu hufunguka zaidi ligi
inavyosonga na kuanza kuangalia mwelekeo sahihi, angalau mechi tano zinaweza
kuwa jibu sahihi.
Ligi nzuri na ya ushindani ni ile ambayo unakuwa huna
uhakika timu ipi itashinda kila zinapokutana. Au nani atashinda kati ya aliye
nyumbani na ugenini.
Pia pamoja na kwamba yamefungwa mabao 12 katika mechi
nane, kuna kila sababu ya wachezaji na hasa washambuliaji kujiuliza mapema
kwamba wamepoteza sana nafasi.
Mechi zote nane zimeonyesha angalau timu nyingi ziliweza
kutengeneza nafasi za kufunga. Waliotakiwa kuzitumia walishindwa kufanya hivyo
jambo ambalo pamoja na kuwa kazi ya mwalimu, lakini linahitaji maboresho
binafsi kwa kila mchezaji.








0 COMMENTS:
Post a Comment