Beki kiraka wa Yanga, Mbuyu Twite amesema amechoshwa
kufungwa na Simba kila mara, hivyo leo vyovyote itakavyokuwa ni lazima timu
yake ishinde.
Simba na Yanga zinacheza mechi ya Ligi Kuu Bara
kwenye Uwanja wa Taifa huku Wanajangwani wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa bao
1-0 katika mchezo wa mwisho katika ligi zilipokutana Machi, mwaka huu.
Twite amesema yeye pamoja na wenzake wamechoshwa na vipigo
kutoka Simba na sasa wameamua kuwageuzia kibao.
Mara ya mwisho kwa Yanga kuifunga Simba ilikuwa
Mei 18, 2013 ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa chini ya
Kocha Ernie Brandts raia wa Uholanzi.
“Msimu
huu lazima tuifunge Simba iwe isiwe kwani tumechoka na uteja, hivyo tumejipanga
kuhakikisha tunashinda, naamini kambi yetu ya Pemba itatusaidia.
“Kikosi chetu kizuri na tunahitaji kushinda
mechi zetu zote zilizo mbele ili kuweza kutetea ubingwa wetu,” alisema Twite
anayemudu kucheza kiungo, pia beki wa kulia hata katikati.
0 COMMENTS:
Post a Comment