Na
Saleh Ally
MSHAMBULIAJI
Mganda, Hamisi Kiiza alikuwa majeruhi. Akalazimika kukaa nje ya uwanja kwa
dakika 180 wakati Simba ikipambana.
Simba
ilicheza dhidi ya Mbeya City na kushinda kwa bao 1-0, Kiiza akiwa amekaa
benchi. Mechi iliyofuata, nayo kwenye Uwanja wa Sokoine, Simba ikalala kwa bao
1-0.
Wakati
Simba inapoteza mechi yake dhidi ya Prisons, Kiiza alikuwa anakamilisha dakika
180 nje ya uwanja. Wakati huo tayari akiwa na mabao matano aliyofunga katika
mechi sita alizokuwa ameichezea Simba.
Maana
yake Kiiza amecheza mechi 6 na kufunga mabao 6 akiwa na wastani wa bao moja
katika kila dakika 90 ambao ni sehemu ya wastani bora zaidi msimu huu.
Kiiza
ni kati ya washambuliaji wenye uzoefu na Ligi Kuu Bara kwa kuwa amecheza Yanga
misimu mitatu, hali inayomfanya awe na uzoefu wa ligi hiyo.
Sasa
jiulize kuhusiana na Simba na safu yake ya ushambuliaji. Kwamba bila ya Kiiza,
hakuna Simba inayofanya kweli.
Asipofunga
Kiiza, hakuna mshambuliaji yoyote wa Simba anayeweza kufunga. Iwe ni mgeni au
mzalendo hakuna anayeweza kutoa msaada kwa kikosi hicho.
Kiiza
amefunga mabao sita kati ya tisa ya Simba. Mengine yamefungwa na viungo,
Justice Majabvi, beki Juuko Murishid na mzalendo pekee aliyefunga bao la Simba
msimu huu hadi sasa, Joseph Kimwaga.
Mganda
huyo amekaa nje, Simba ikashinda kupitia bao lililofungwa na beki. Mechi
iliyofuata washambuliaji hawakufunga tena na wakapoteza kwa bao 1-0 dhidi ya
Prisons.
Kiiza
amerejea, washambuliaji au viungo wengine hawakufunga tena. Hadi Kiiza amefunga
na kuipa Simba pointi tatu nyingine, sasa imepanda hadi nafasi ya nne ikiwa na
pointi 18!
Wengine
wako wapi? Wanafanya nini na kwa nini hawafungi? Au ndani ya Simba kuna tatizo
linalofanya wasiwe katika kiwango kizuri?
Mfano
inawezekana hata wanaocheza hawana furaha. Kwani inawezekana tukawalaumu
wachezaji lakini kuna kitu kinawakera au hawana furaha. Kama ni hivyo,
wanapaswa kumalizana na uongozi au kusema hadharani maana lawama zitaendelea
kudondoka kwao kwa kuwa kufunga si jukumu la uongozi.
Kwa
uongozi kama kuna tatizo, mfano kuchelewa kwa mshahara au kuna mfarakano wa
chinichini kati ya wachezaji basi kuna kila sababu ya kuumaliza.
Hivi
karibuni nimesikia wachezaji wa Simba wakiwa kambini walitaka kuzichapa.
Najiuliza kwa nini ilikuwa hivyo na ugomvi ulilenga kipi hasa?
Kama
ungekuwa ni ugomvi wa uwanjani ungesema ni presha ya mchezo. Lakini
wanapogombana kambini, basi kuna shida na hili ni jukumu la uongozi
kulishughulikia hili suala la kwa uhakika ili kurejesha hali ya amani na
upendo.
Hakuna
mafanikio sahihi katika sehemu yoyote kama hakuna upendo. Kawaida upendo
unasimamiwa na uongozi na viongozi wengine ndani ya timu, mfano benchi la
ufundi ambalo linaongozwa na Mwingereza Dylan Kerr.
Mwisho
nikumbushe, uongozi wa Simba kupitia kamati zake za usajili, ufundi na ile kubw
ya utendaji lazima wakubali kwa mara nyingine wamechemsha katika usajili na
hasa safu ya ushambuliaji.
Safu
ya ushambuliaji ya Simba si hatari na inatembelea nyota ya Kiiza. Hivyo ni
kufanya maamuzi magumu na ikiwezekana kuisafisha kabisa au kufanya mabadiliko
makubwa na upembuzi wa nini kifanyike lazima uwe umeanza sasa na si kusubiri
hadi mwishoni halafu wakurupuke tena, mwisho ndiyo kuangukia kwa watu kama
akina Pape N’daw ambao wanakwenda uwanjani wakiwa na ‘power bank’ lakini bado
hawana msaada wowote zaidi ya kuwatia aibu na kuanzisha vichekesho tu!
0 COMMENTS:
Post a Comment