Mwenyekiti
wa zamani wa Simba ambaye pia alikuwa ni Mwenyekiti wa Chama cha Siasa cha National
League for Democracy (NLD), mzee Emmanuel Makaidi, 74, amefariki dunia jana
kwenye Hospitali ya Nyangao mkoani Lindi.
Kaimu
mganga mkuu wa hospitali hiyo, Betram Makota, ameliambia Championi Ijumaa:
“Mzee Makaidi aliletwa hapa akiwa amezimia, tukiwa katika harakati za kumtibu
akafariki dunia.”
Mke
wa marehemu, Modesta Makaidi, naye alisema: “Marehemu alikuwa akisumbuliwa na
shinikizo la damu, alizidiwa na tulipompeleka hospitali akafariki dunia.”
Mzee
Makaidi alikuwa mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na pia
alikuwa Mgombea Ubunge wa Jimbo la Masasi kwa Tiketi ya NLD.
Licha
ya kuwa mwanasiasa, Mzee Makaidi amewahi kushika nafasi kadhaa za uongozi
katika Klabu ya Simba ambapo mwaka 1969 alikuwa katibu mwenezi, mwaka 1973
alikuwa katibu mkuu na mwaka 1983 alikaimu nafasi ya mwenyekiti akichukua
nafasi ya Joachim Kimwaga.
Mwenyekiti
wa zamani wa Simba, Hassan Dalali amesema: “Huyu ni Simba mwenzetu na amewahi
kushika nafasi kadhaa za uongozi licha ya kuwa mwanasiasa, huu ni msiba wa
Simba na wanamichezo wote nchini.”
Afisa
Habari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tumaini Makene,
aliliambia gazeti hili kuwa, mipango ya mazishi ingepangwa jana usiku kwa
pamoja kati ya viongozi wa Ukawa na familia ya marehemu.
0 COMMENTS:
Post a Comment