Na Saleh Ally
UKIZUNGUMZIA
mchezo wa ngumi za kulipwa hapa nyumbani, hakuna ubishi bondia namba moja
utamtaja Francis Cheka ambaye ndiye tegemeo kubwa kwa Watanzania wengi.
Cheka ambaye
mama yake ni raia wa Msumbiji, amekuwa gumzo kutokana na kufanya vizuri katika
mchezo huo tangu akiwa katika ngumi za ridhaa ingawa yeye analia kwa kusema
pamoja na yote, bado ni masikini wa kutupwa.
Anasema
amepigwa ngumi nyingi sana, lakini maisha yake yamekuwa na ahueni tu, kamwe
hayalingani hata kidogo na sifa au ukubwa wa jina lake katika jamii.
Katika
mahojiano na Cheka amesema amekuwa akiishi maisha ya shida
sana tofauti na watu wengi wanavyofikiria, hali ambayo imekuwa ikimpa wazo la
kuachana kabisa na mchezo wa ngumi.
SALEHJEMBE:
Kwa nini unafikiri uache ngumi Cheka?
Cheka: Naumia
sana ndugu yangu, najiona najitoa kwa ajili yangu, taifa langu lakini sina
thamani na maisha yangu ni magumu sana.
SALEHJEMBE: Unafikiri ukiacha ngumi katika kipindi hiki utafanya kazi ipi?
Cheka: Nina
kiwanda cha kusaga plastiki ambacho nilikinunua kwa Mhindi mmoja hivi. Ingawa
nako ninapata shida kubwa sana kwa kuwa inahitajika Sh milioni mbili tu ili
mambo yakae sawa, lakini siwezi kupata pia.
SALEHJEMBE: Ungeweza kwenda benki na kukopa ili uendeleze biashara, umeshindwa hilo?
Cheka: Nimewahi
kujaribu, lakini ikawa shida kubwa kwa kuwa kipato changu hakieleweki, nusura
nyumba yangu iuzwe, mke wangu akaokoa jahazi.
SALEHJEMBE:Ilikuwa shilingi ngapi? Ulishindwa kulipa hadi wakachukua hatua hiyo?
Cheka:
Nilikopa Sh milioni tano, ikawa imebaki Sh laki saba tu. Sikuwa nimeshindwa,
ila nilichelewesha rejesho kwa miezi mitatu. Halikuwa lengo langu, lakini
kipato changu ni duni kabisa.
SALEHJEMBE:Wewe ni bondia mkubwa Cheka, unapocheza unalipwa fedha nyingi au matumizi yako
hayana nidhamu?
Cheka:
Unaweza kufikiri nalipwa fedha nyingi, lakini hapa nyumbani hakuna heshima hiyo
maana mapromota hawatoi fedha nyingi, ingawa siwalaumu sana maana nao wanakosa
wadhamini.
SALEHJEMBE: Kawaida unalipwa kama kiasi gani kwa pambano moja?
Cheka: Malipo
yanatofautiana kulingana na pambano, lakini juu angalau Sh milioni tano.
Usisahau kuna maandalizi, nalipia kambi, chakula pia ni lazima niwe na watu
zaidi ya wawili. Maandalizi yanahitaji muda, angalau zaidi ya wiki mbili, tatu.
SALEHJEMBE:Je, unaweza kusema mchezo wa ngumi haujakusaidia kabisa?
Cheka: Kamwe
siwezi kuinua mdomo na kusema hivyo, umenisaidia kwa mengi, umenikutanisha na
marafiki wengi sana lakini naona jina linapaa kuliko mafanikio halisi.
SALEHJEMBE: Umewahi kupata gari baada ya kushinda pambano la ngumi, lakini sasa unatembea
kwa miguu tu, vipi?
Cheka: Kweli,
nilipata gari aina ya Toyota Corolla. Nililazimika kuliuza baada ya kuona baba
yangu akiteseka kwa kuishi kwenye nyumba ya kupanga kule Kinondoni. Alikuwa na
kiwanja Mbagala, nimejengea nyumba ya vyumba vitatu, angalau anaishi kwake.
Lakini bado
sijaridhika, maana nyumba haiko katika hali nzuri, haina hata madirisha ndiyo
napambana. Baba yangu ni masikini, hajiwezi na haoni, macho yake yamepoteza
nuru, ni kipofu.
SALEHJEMBE: Taarifa zinasema umevuliwa mataji ya dunia, nini hasa tatizo?
Cheka: Kweli
nimevuliwa ubingwa, taji la kwanza la WBF ambalo nilimpiga Mmarekani nilivuliwa
kwa kuwa nilikwenda kupigana Urusi katika pambano lisilokuwa na ubingwa,
nikapoteza.
Nimevuliwa
mataji mengine matatu, jumla nimelipiwa mikanda minne bila kuitetea.
SALEHJEMBE:Kama ulijua kufanya vile, vipi ulikubali kwenda kupigana Urusi?
Cheka: Ndugu
yangu, ndicho ninachokueleza, njaa. Nitaacha vipi fedha wakati nina nafasi ya
kwenda kupigana? Hapa nyumbani pambano halijaandaliwa.
SALEHJEMBE: Mataji mengine pia umevuliwa, huoni kama ni tatizo kwako?
Cheka: Si
tatizo, katika hii mikanda mingine miwili, sikuwa na pambano. Hakuna promota
aliyejitokeza kuandaa na wenyewe wanalalamika hawana fedha za kutosha.
SALEHJEMBE:Hawana fedha za kuandaa mapambano, kivipi?
Cheka: Unajua
pamoja na fedha zao za mfukoni, mapromota nao wanahitaji wadhamini. Nashangazwa
sana na makampuni kudharau ngumi za kulipwa jambo ambalo si zuri, nafikiri
wabadilike sasa. Mchezo wa ngumi unapendwa sana.
SALEHJEMBE: Unafikiri umeliletea taifa letu sifa kwa kiasi gani?
Cheka: Kama
Cheka nimeleta heshima kubwa sana kwa juhudi zangu binafsi. Nimepigiwa wimbo wa
taifa, usisahau nimewapiga mabondia kutoka Marekani, Azerbaijan, Malawi, Brazil
na kwingine. Mimi ndiye bondia niliyepigiwa zaidi wimbo wa taifa.
SALEHJEMBE:Kuna taarifa ulipewa bati na mifuko ya saruji na serikali baada ya kutwaa
ubingwa wa dunia, lakini ukaziuza. Kwa nini ulifanya hivyo?
Cheka: Ndugu
yangu watu wazushi sana, hizo bati zilitakiwa kuwa 130, hadi sasa sikuwa
nimepewa na hata siku ya tuzo za Taswa nilimkumbusha Rais (Jakaya) Kikwete
kwamba bati zangu bado sijapewa.
Kweli Joel
Bendera alinipa mifuko 80, pia nikapewa kiwanja. Mabati hadi sasa bado
sijapewa, ninaamini Rais Kikwete atafanya hivyo.
SALEHJEMBE:Matarajio ya wengi, ilikuwa ni lazima utapigana pambano dhidi ya bondia wa nje.
Umerudi kupigana na Thomas Mashali tena, hauoni kama unashuka?
Cheka:
Nitafanyaje sasa, maana hakuna mapromota wanaoleta mapambano ya nje. Nimekuwa
nikishinda karibu kila pambano, lakini sipati mapambo ya nje. Nitakachofanya ni
kupambana nipate fedha ya kuendeleza kiwanda changu lakini namtwanga Mashali
ili kulinda heshima yangu.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment