REKODI zinaonyesha Simba haijawahi kuifunga
Mbeya City katika historia yake, pia Yanga haijawahi kuifunga Azam FC katika
Ligi Kuu Bara ndani ya misimu miwili iliyopita.
Nayo Simba msimu wa 2013/14 ilianza kwa kutoka
sare ya mabao 2-2 na Mbeya City na ilipoenda Mbeya ikatoka sare tena ya bao
1-1, msimu uliopita Simba ilianza kwa kufungwa nyumbani mabao 2-1 na jijini
Mbeya ililala mabao 2-0.
Makocha na wachezaji wa Simba na Yanga,
hawataki tena masihara wameshtuka na leo Jumamosi wanataka timu zao kuvunja
mwiko huo wa misimu miwili sasa.
Jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa,
Yanga itacheza na Azam na tayari Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm
amebadilisha vitu kadhaa kikosini ili apate ushindi.
Pluijm abadili kikosi makusudi
Kwa kujua kwamba Azam ina winga mwenye kasi
Farid Mussa, Pluijm amepanga kumtumia Juma Abdul katika beki ya kulia badala ya
Mbuyu Twite pia amewaingiza kikosi cha kwanza Malimi Busungu na Salum Telela
kuendana na kasi ya Azam.
Mbali ya Twite wachezaji wengine walioondolewa
kikosi cha kwanza ni Haruna Niyonzima na Simon Msuva, lengo ni kupata ushindi
dhidi ya Azam, leo.
“Nimeshamaliza maandalizi yangu kwa mechi na
Azam, hii si timu ndogo ni mechi iliyojaza ufundi na ushindani ni mkubwa hivyo
kuna mabadiliko nimeyafanya nadhani yatatusaidia,” alisema Pluijm katika
mazoezi ya mwisho jana asubuhi.
Hata hivyo, Azam kidogo imeonekana kuwa kimya
kuelekea mchezo huo lakini Kocha Stewart Hall ambaye hataki mazoezi yake
yahudhuriwe na mtu yeyote yule, alisema; “Tutapambana tukae kileleni.”
Wachezaji wawili wa Azam, Allan Wanga na Jean
Baptiste Mugiraneza ‘Migi’ tayari wamerejea kutoka katika majukumu ya timu za
taifa ili kuivaa Yanga. Wanga ametokea Kenya na Migi alikuwa Rwanda.
Vita ya pointi zaidi kileleni
Yanga na Azam, zote zina pointi 15 lakini
Wanajangwani wapo kileleni kwa kuwa na mabao mengi ya kufunga ambayo ni 13 huku
Azam ikiwa nayo tisa tu.
Pia Yanga imefungwa bao moja tu, wakati Azam
imeruhusu mabao mawili. Mchezo wa Simba na Mbeya City wenyewe umebaki katika
rekodi zaidi kwani Wekundu wa Msimbazi wapo nafasi ya tatu na pointi 12 huku
wapinzani wao wakiwa wa 13 na pointi nne tu.
Simba nayo imekataa
Kocha wa Simba, Dylan Kerr na nahodha wake
Mussa Mgosi kwa pamoja wamesema sasa ‘nooo!!’ wakimaanisha hawatakubali kukosa
pointi ugenini kwenye Uwanja wa Sokoine.
“Tupo hapa kwa zaidi ya wiki sasa, hatutaki
kupoteza mchezo huu japokuwa nasikia Simba haijawahi kushinda hapa, wapinzani
wetu wana timu nzuri lakini nasi tutapambana kupata pointi,” alisema Kerr.
Kuelekea mchezo huo, kiungo wa zamani wa Simba,
Haruna Moshi ‘Boban’ ametua rasmi katika kikosi cha Mbeya City kuitumikia kwa
mujibu wa mkataba wake tangu awali.
Kwa upande wake, Mgosi alisema: “Najua Mbeya
City wana Boban na Kaseja (Juma), hawa ni wazoefu lakini sipendezwi na rekodi
ya Simba kutoifunga timu hii, tutajitahidi tushinde.”
Kuelekea mchezo huo, mashabiki wa Mbeya City
waliweka ulinzi kwenye Uwanja wa Sokoine na kutoruhusu mtu yeyote kutazama
mazoezi yao wakihofia kuibiwa mbinu zao.
Kocha wa Mbeya City anayekaimu nafasi ya Juma
Mwambusi aliyeenda Yanga, Meja Mstaafu, Abdul Mingange alisema; “Naijua Simba
inaishiwa na pumzi kipindi cha pili, nitawakamata hapohapo wala hakuna tabu,
tuombe wachezaji wetu wawe wazima Jumamosi (leo).”
Viwanja
vingine;
Leo Jumamosi, Majimaji itacheza na African
Sports Uwanja wa Majimaji, Ndanda FC na Toto Africans Uwanja wa Nangwanda
Sijaona, Mtwara, Stand United na Prisons Uwanja wa Kambarage Shinyanga na Tanga
kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Coastal Union itacheza na Mtibwa Sugar.
Kesho Jumapili, Mgambo Shooting itacheza na
Kagera Sugar, Mkwakwani na Mwadui FC itacheza na JKT Ruvu Uwanja wa Mwadui
Complex.
0 COMMENTS:
Post a Comment