Na Saleh Ally
NIANZE na kukumbusha, Septemba 29, Yanga
ilikuwa mgeni wa Simba kwenye Uwanja wa Taifa. Mechi hiyo ilimalizika kwa
wenyeji kulala kwa mabao 2-0.
Halafu, Simba ilikuwa mgeni wa Mbeya City
katika mechi iliyopigwa Oktoba 17 kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. Wageni
wakaibuka na ushindi wa bao 1-0.
Tangu mechi ya Simba dhidi ya Yanga
imechezwa, leo tayari ni siku 31, mwezi mmoja na siku moja.
Halafu tangu ichezwe mechi ya Simba ikiwa
ugenini dhidi ya Mbeya City, leo zimetimia siku 11. Hadi Jumamosi, zitakuwa ni
wiki mbili.
Hesabu zote hizi ni kwa ajili ya kutaka
kukuonyesha kiasi gani Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeamua kukaa kimya
kufumbia madhambi bila ya kujali muda unakwenda au la.
Nasema limefumbia macho madhambi tena ya
wazi kwa kuwa karibu kila mpenda soka aliona matukio mabaya kabisa
yaliyojitokeza ambayo ni taswira mbaya na isiyokuwa na manufaa kwa mpira wa
Tanzania.
Katika mechi Simba dhidi ya Yanga,
mshambuliaji Donald Ngoma raia wa Zimbabwe alimpiga kiwiko tena kibaya beki
Hassan Kessy wa Simba ambaye alianguka na kutolewa nje kwa ajili ya kutibiwa.
Picha za video zipo zikionyesha Ngoma
akifanya ujinga huo. Lakini ajabu TFF hadi sasa imekaa kimya na haionyeshi
kuchukizwa na hali hiyo!
Hali kadhalika tukio la Mbeya ambalo nalo
lipo katika picha za video, ikionekana wazi kabisa Juuko akimtwanga kiwiko
mchezaji wa Mbeya City ambaye hakika katika hali ya kawaida, inaonekana
aliumizwa!
Tayari nimeona Simba na Mbeya City kila
upande umepeleka malalamiko TFF. Lakini ninachoona hakukuwa na sababu ya
shirikisho hilo kusubiri malalamiko haya, kitu kibaya zaidi wameendelea kukaa
kimya!
Suala la nahodha wa Coastal Union, Juma
Nyosso kumdhalilisha nahodha wa Azam FC, TFF ililifanyia kazi kwa kutumia ile
kamati ya saa 72 ambayo ilichukua adhabu kali hadi ikalalamikiwa na wadau
wengi.
Adhabu ilikuwa kali na ya haraka hadi
ikawashangaza wengi. Suala la udhalilishaji halikuwa zuri na niendelee
kulikemea kwamba ni baya na Nyosso anapaswa ajifunze.
Lakini hapohapo, najiuliza TFF haioni kuwa
si sahihi mchezaji mmoja kukusudia kumuumiza au kumtoa mwenzake uhai kwa
makusudi halafu jambo lionekane ni la kawaida? Kwani ile kamati ya saa 72 ni
kwa ajili ya wadhalilishaji tu?
Wakati najiuliza maswali tata, kwamba au TFF
wana hofu ya kutoa adhabu kwa Ngoma au Juuko kwa kuwa ni wachezaji kutoka
katika klabu kubwa?
Halafu najiuliza tena, huenda TFF wanakuwa
waoga kutoa adhabu kwa wachezaji wa kigeni kwa kuwa Ngoma anatokea Zimbabwe na Juuko
ni raia wa Uganda!
TFF wasisababishe wadau waanze kuzungumza
mambo ambayo si sahihi au watetezi wa mambo waanze kufikiria waliofanya hivyo
ni wageni na waliofanyiwa ni Watanzania!
Huu ndiyo wakati TFF inapaswa kuitisha
kamati husika na mara moja ikae na kutoa uamuzi kwa kuwa kila kitu kipo wazi.
Sitaki kuingia katika masuala ya ushabiki
kama isivyo kawaida yangu. Ila nasisitiza, Ngoma na Juuko wamefanya makosa tena
ni ya kipuuzi na wanastahili adhabu ili iwe mfano kuanzia kwa wachezaji wa
kigeni na wazalendo wengine.
Kumekuwa na uwazi mkubwa katika suala hilo
kwa kuwa ushahidi unajitosheleza. TFF inapaswa kulifanyia kazi suala hilo kwa
ajili ya kuondoa ukakasi na hakutakuwa na namna zaidi ya wachezaji hao wawili
kuadhibiwa na kukumbushwa kwamba wamekuja kucheza soka, wangetaka Kung Fu au
karate, wangeweza kuchagua njia nyingine.
Pia nashauri, TFF inapaswa kuwa inachukua
hatua haraka kwa matukio kama hayo ili kuwaonyesha wachezaji wenye nia mbaya na
afya za wengine kwamba anayefanya hivyo, adhabu kali itafuatia kwa ajili yake.
0 COMMENTS:
Post a Comment