Baada ya mchezo wa leo baina ya Simba dhidi
ya Coastal Union, uongozi wa Simba utakutana kujadili mwenendo mbovu wa timu
hiyo, shutma zinazowakabili pamoja na ishu nzima za usajili wa wachezaji wapya.
Pamoja na kikako hicho, tayari Simba ipo katika harakati ya kupata washambuliaji watakaobadili gia ya kikosi chao.
Washambuliaji hao wa kigeni ni Warundi, Kevin Ndayisenga wa AO Bujumbura na Laudit Mavugo wa Vital’O, Mganda, Brian Majwega (KCCA) na kumrejesha Mkenya, Paul Kiongera waliyemtoa kwa mkopo KCB.
Kikao hicho pia kitahusisha benchi la ufundi
la timu hiyo lililo chini ya kocha Muingereza, Dylan Kerr, kwa ajili ya kujibu
baadhi ya maswali ya uongozi kwa ajili ya kikosi hicho pamoja na mikakati yake.
Simba imefikia uamuzi huo baada ya kuyumba
kwa timu hiyo katika mechi zake za mwisho na kusababisha matokeo ya kukamata
nafasi ya tano wakiwa na pointi 15 huku wakiachwa na mahasimu wao, Yanga walio
kileleni kwa pointi 19.
Kamati mbalimbali zitakutana na kujadili
masuala yake kabla ya kukutana na kamati ya utendaji na kuwasilisha
walichokiona kisha kamati hiyo kulivaa benchi la ufundi na kujua mbivu na
mbichi, ikidokezwa pia hata hatma ya Kerr itabainika kupitia kikao hicho.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amefafanua
baadhi ya vitu kuhusiana na suala hilo.
“Kuna mambo mengi yamejiri hapa katikati,
lakini kitafanyika kikao cha kamati ya utendaji na benchi la ufundi kwa ajili
ya kuangalia mambo mengi kwamba kwa nini timu inafeli; tulianza vizuri na sasa
mambo yamebadilika. Tutalisikiliza benchi linasemaje kuhusiana na hilo.
“Kuhusu usajili tutazungumza pia kupitia
kikao hicho, tutapata listi ya wachezaji au nafasi zinazohitajika kwa ajili ya
dirisha dogo na sisi tutatekeleza, nafikiri hiki kikao cha baada ya mechi na
Coastal ndiyo kitatoa mwanga wa mambo mengi, yatapatikana na majibu ya usajili
wa kina Mavugo (Laudit) na hao wengine wanaotajwa kutua Simba,” alisema Poppe.
0 COMMENTS:
Post a Comment