November 14, 2015


Na Saleh Ally
GUMZO la Kocha Jose Mourinho ni kubwa, kikosi chake cha Chelsea ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu England kimeendelea ‘kuchekesha’ kila kukicha.

Mourinho ameingia kwenye rekodi ya chini kabisa baada ya kupoteza mechi saba katika msimu mmoja. Hii haijawahi kumtokea Mourinho katika misimu 15 ya kazi yake ya kufundisha.

Vipigo saba ndani ya msimu kumeifanya Chelsea kuwa bingwa mtetezi wa ‘hovyo’ kabisa kwa kuwa bado pointi tatu tu waingie kwenye kundi la wanaowania kuepuka kuteremka daraja.

Sasa Chelsea inashikilia rekodi ya bingwa mtetezi aliyepoteza mechi nyingi zaidi msimu aliokuwa akitetea na hasa mzunguko wa kwanza. Haina kichwa wala miguu.

Maswali ni mengi, kwamba tatizo hasa la Chelsea ni lipi? Kila mmoja anaweza kuwa na yake kwa kuwa sasa ni kipindi cha matatizo, lakini yafuatayo ni kati yaliyochangia kuiangusha Chelsea;

Ivanovic si yule…
Kati ya wachezaji waliokuwa wakiifanya Chelsea kuwa imara ni beki Branislav Ivanovic akitokea kulia. Pamoja na ukabaji wa uhakika, krosi zake nyingi zilisaidia kuzaa mabao au mwenyewe alifunga vizuri kabisa.

Msimu huu anaonekana amepotea na kiwango chake ni cha kubahatisha.

Kuyumba kwa John Terry
Nahodha wa Chelsea, John Terry amekuwa mhimili mkubwa wa ulinzi na uimara kwa kikosi kwa jumla. Kuporomoka kwa kiwango chake kunamfanya asiwe msaada tena na sasa kikosi kinapoteza mwelekeo katika ulinzi. Hata anapokuwa nje wanaopewa nafasi yake hawaitendei haki kwa usahihi. Hafungi tena katika mechi muhimu, huenda umri mkubwa au amechoka tayari.

Kumkosa Stone
Baada ya Mourinho kumkosa beki wa Everton, John Stone hili lilikuwa tatizo jingine msimu huu. Ndiye aliyeonekana ni mrithi sahihi wa Terry. Sasa ni pengo linaloonekana halizibiki na hiyo inakuwa ni sehemu ya Chelsea kukosa uimara.

Kuumia kwa Thibaut Courtois
Wakati msimu uliopita Chelsea ilipochukua ubingwa, kipa Thibaut Courtois alionekana ndiye mhimili mkubwa katika safu ya ulinzi. Kuumia kwake kumeifanya Chelsea ipoteze mambo mengi ya uhakika katika kujilinda.

Mourinho alikubali kumuuza Petr Cech kwa kuwa mkononi alikuwepo Courtois, ambaye sasa ni majeruhi.

Kumuuza Petr Cech kwa Arsenal
Mourinho alikubali kumuuza Petr Czech kutokana na uhakika aliouonyesha Mbelgiji Courtois.

Alipoumia, inaonekana wazi hakuna ambaye angekuwa mkombozi wa Mourinho langoni zaidi ya kipa huyo kutoka Jamhuri ya Czech. Sasa anatamba Arsenal na kuthibitisha kweli Mourinho alikosea.

Cesc Fabregas hayuko sawa
Imekuwa vigumu kwa watu wengi kuona kiungo Cesc Fabregas hayuko katika kiwango chake sahihi.

Mhispania huyo ameporomoka, ameshindwa kuwa kama ilivyokuwa msimu uliopita, jambo ambalo linachangia kuiangusha Chelsea hasa inapokuwa inashambulia. Si mtu sahihi wa mipango tena.

Kuna shida kwa Eden Hazard
Ukiona anakimbia na mpira na kutoa pasi unaweza kuamini bado ni hatari, lakini ukweli mchezaji huyo bora wa mwaka kwa upande wa vijana kupitia tuzo ya PFA msimu uliopita, hayuko vizuri.

Kukimbia vizuri pekee si usahihi au majibu yanayotakiwa, takwimu zinamshtaki Hazard maana hana bao hata moja na ametoa pasi mbili tu zilizozaa mabao.

Unakumbuka msimu uliopita, alifunga mabao 21 kwa Chelsea. Alikuwa msaada mkubwa kwa Chelsea kutwaa ubingwa England hadi akapaa kuwa kundi la akina Lionel Messi na Cristian Ronaldo. Yuko wapi sasa?

Namba tisa bado haijakaa vizuri
Diego Costa anasifika kwa utukutu, mbabe na anawachanganya mabeki lakini bado hajakaa vizuri katika ufungani. Loic Remy naye bado hajasomeka vizuri.

Usajili mpya wa Mourinho aliyeamua ‘kujaribu’ kwa Radamel Falcao nao unaonekana kugonga mwamba na sasa hisia ziko hivi. Didier Drogba bado alistahili kubaki msimu mmoja kuituliza safu ya ushambulizi ya Chelsea.

Kumfukuza Daktari Eva Carneiro
Mourinho amechangia kuondoka kwa daktari wa timu, Eva Carneiro, kisa aliingia kumtibu Hazard uwanjani wakati timu hiyo ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Swansea.

Hapa kuna maswali mengi. Je, wachezaji wameumizwa sana kwa kuwa alikuwa akimsaidia mwenzao? Heshima kubwa ya daktari huyo mwanamke. Hivyo wana kinyongo hata kama hawaonyeshi.


Imeonyesha Mourinho alivuka mstari. Maana amezoea kuwatetea wachezaji wake au watu wake wa Chelsea hadi mwisho. Safari hii akawa ndiye anayewatandika jambo ambalo halikuwa sahihi kwa kuwa Eva alikuwa msaidizi wa watu ambao wanaumia kwa ajili yake.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic