November 14, 2015


Na Saleh Ally
KOCHA Msaidizi wa Simba, Selemani Matola ameamua kubwaga manyanga na tayari sababu kadhaa zimeelezwa, likiwemo suala la kutoelewana na bosi wake, Muingereza, Dylan Kerr.

Matola ameamua ‘kuepusha msongamano’, sasa si mfanyakazi tena wa Simba na sababu ni hiyo, kwamba hawaelewani na Kerr.

Ufuatiliaji wangu umeng’amua mambo mengi sana ndani ya Simba. Kwamba ilifikia Matola na Kerr hawakuwa wakizungumza tena na kila mmoja alikuwa akimshutumu mwenzake.

Kuna taarifa Kerr alimshutumu Matola kuacha kufanya kazi yake ya ukocha na kugeuka shushushu wa baadhi ya viongozi waliokuwa wakishinikiza baadhi ya wachezaji wapangwe kwa matakwa ya viongozi hao.

Lakini Matola naye anamshutumu Muingereza huyo kuwa hasikilizi ushauri, hapendi kukosolewa na imefikia hatua anamchonganisha yeye na wachezaji. Lengo ni kumsogeza mbali na wachezaji.

 Kwamba wakati mwingine anafanya vikao na wachezaji na kumuondoa Matola, au akipanga listi, kocha huyo msaidizi naye anaijua wakati wanataarifiwa wachezaji!

 Kama kweli Matola alikuwa ni shushushu kama tuhuma zilivyosukumwa kwake, basi hakuwa sahihi hata kidogo, tena ni jambo baya sana na kama kuna hao viongozi wenye tabia hizo wapo Simba, wao ndiyo watakuwa wachawi wa kwanza siku ikianguka.

 Angalia leo, wako wanaojua mengi ndani ya Simba, lakini uwezo wao mdogo na wakati mwingine wanataka kumfundisha kocha.

Matola ameamua kuondoka, ukiachana na shutuma hizo, naona kama alichelewa sana kuondoka Simba na sasa amefunguka macho.

 Matatizo wakati mwingine ni jambo zuri, hasa kama hayakupi ulemavu au maumivu ya mwili kama majeraha.

Kama ni maumivu kama anayoyapata Matola ya kuona alikuwa na ndoto na Simba, halafu zimekatishwa katikati, bado anaweza kufanikiwa sana.

 Matola ni kati ya makocha wanaoweza kuwa hazina kubwa ya Tanzania hapo baadaye. Lakini alikuwa ni sawa na Watanzania wengi sana ambao wamekuwa waoga wakihofia kujaribu.

 Amekuwa katika kundi la Watanzania wanaoogopa lawama. Huenda aliona sawa kuwa chini au kocha msaidizi kusudi siku mambo yakiwa mabaya, yeye asihusike au aonekane bosi wake ndiye aliyekosea.

 Inawezekana pia, Matola aliona kuendelea kubaki Simba kama kocha msaidizi ni bora zaidi kuliko akiwa kocha mkuu katika timu nyingine ya Ligi Kuu Bara au daraja la kwanza.

Kumbuka amekuwa chini ya makocha wazungu zaidi ya watatu sasa. Kivuli ambacho alitakiwa kukivua mapema kwani kama mafunzo, yalitosha na Simba walipaswa kumuamini baada ya kuondoka kwa Goran Kopunovic. Hawakumwamini! Hapo ndipo alitakiwa kujiamini yeye binafsi.

 Sasa ndiyo wakati wa Matola kukua, kupima uwezo wake na kuonyesha anaweza. Kama atafanikiwa, basi bora aanze na timu ya daraja la kwanza kupambana kwenda ligi kuu.

 Tayari Matola alishaonyesha uwezo mkubwa kwa kuisaidia timu ya vijana ya Simba kubeba ubingwa wa Kombe la Banc ABC tena kwa kuzifunga timu kama Azam FC na Mtibwa Sugar. Sasa leo anahofia nini au kipi?

 Kama ingekuwa ni ushauri, basi ningemshauri Matola kuondoka kabisa ligi kuu. Arejee daraja la kwanza, kwani kwa muda alionao, bado anahitaji kujifunza mengi.

 Kama ishu ni maslahi, basi analazimika kutengeneza uwezo zaidi. Siku akiipandisha timu, au akiitwa na Simba basi awe kocha mkuu na inawezekana akafanya mengi makubwa akiwa kiongozi mkuu katika kikosi.

 Inawezekana kweli Kerr alikuwa akiona anachotaka kufanya Matola kinajenga zaidi au kitampa sifa sana, kama bosi asiyekubali, akaona Mtanzania ‘anamharibia’.

 Bado pia inawezekana huenda Matola kutokana na alichokuwa akikiamini hakupenda kizuiwe hata kama hakikuwa kizuri sana kwa kuwa alijiamini na alikiamini alichokuwa akikitoa.
 Akiwa kocha mkuu wa timu ya daraja la kwanza, atakuwa na uwezo wa kuona anachokiamini kinavyofanikiwa au kufeli na hapo atajifunza zaidi kuliko kila anachokitoa anasubiri bosi akipitishe.


 Nenda tu Matola, huu si wakati wa uoga tena na ukiweza, tafuta timu ya daraja la kwanza, siku ukirejea ligi kuu, basi utakuwa na uwezo wa kwenda juu zaidi kuliko ulivyokuwa umejificha kwenye kivuli cha makocha wazungu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic