Kocha Mkuu wa timu ya Taifa Tanzania
‘Taifa Stars’ inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Charles
Boniface Mkwasa amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya
Algeria kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi.
Akiongea katika mkutano na waandishi wa
habari leo, Mkwasa amesema wamejiandaa kuhakikisha wanafanya vizuri katika
mchezo huo, wanajua Algeria ni miongoni mwa timu bora Afrika, lakini hilo
halitawazuia kuibuka na ushindi.
“Katika mpira wa sasa duniani hakuna timu
kubwa wala timu ndogo, lolote linaweza kutokea, sisi tuna nafasi ya kufanya
vizuri tukiwa katika uwanja wa nyumbani na washabiki wetu” alisema Mkwasa.
Aidha Mkwasa alisema wamefanya mazoezi
kwa pamoja kwa takribani siku 10, vijana wapo katika hali nzuri, hakuna
majeruhi vijana wote wapo katia hali nzuri na timu imefanya mazoezi ya mwisho
leo asubuhi kabla ya kushuka dimbani kuwakabili Mbweha wa Jangwani.
Mwisho Mkwasa amewaomba watanzania
kujitokeza kwa wingi uwanja wa Taifa kuja kuwapa sapoti vijana watakapokuwa
wanapeperusha bendera ya Tanzania.
Mechi kati ya Tanzania dhidi ya Algeria
kesho Jumamosi itaanza saa 10:30 jioni katika uwanja wa Taifa jijini Dares
salaam.
0 COMMENTS:
Post a Comment