November 21, 2015


Wakati Simba wakiendelea na usajili wa dirisha dogo la usajili msimu huu wa Ligi Kuu Bara, Yanga wenyewe wamesimamisha zoezi hilo wakisubiri droo ya Ligi ya Mabingwa Afrika (Caf).


Dirisha dogo la usajili wa ligi kuu limefunguliwa tangu Novemba 15 na litafungwa Desemba 15, mwaka huu, ili kuzipa timu nafasi ya kusajili kuboresha vikosi vyao.

Yanga itashiriki michuano hiyo ya Caf, baada ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu uliopita huku Azam FC ikitwaa nafasi ya pili ambapo itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika, mwakani.

Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha, alisema mara baada ya droo hiyo kufanywa na kujua timu watakazokutana nazo, ndipo watajua wanatakiwa kusajili kwa namna gani.

Tiboroha alisema, ni ngumu kwao kufanya usajili katika kipindi hiki ambacho hawajui wataanza na timu za nchi ipi katika michuano hiyo mikubwa ambayo inahitaji umakini katika usajili wao.

Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa Caf, droo hiyo imepangwa kufanyika Desemba Mosi, mwaka huu, kipindi ambacho usajili utakuwa ukiendelea nchini.

“Kama unavyojua, Yanga tupo kwenye maandalizi ya ligi kuu na michuano mikubwa ya kimataifa Afrika, hivyo tunahitajika kuwa makini katika usajili wetu katika kuendana na kasi.

“Hivyo kama uongozi hivi sasa tumesimamisha usajili kwa muda, tukisubiria droo ya Caf ili kujua timu tutakazopangwa nazo katika hatua ya awali, halafu tutajua aina ipi ya wachezaji tuwasajili ambao tunaamini tukiwa nao wataisaidia Yanga kimataifa.

“Basi mara baada ya kutoka droo tukiona kuna mahitaji ya wachezaji wa kuwaongeza, basi tutasajili wachezaji wa hapa nchini wazawa pekee na siyo wa kimataifa kutokana na idadi ya wachezaji wa kimataifa kukamilika,” alisema Tiboroha.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic