Na Saleh Ally
KATIKA sehemu mbili za mwanzo za makala haya,
nilianza kugusa kuhusiana na wale waliokuwa wakipiga kelele na kuidhihaki Taifa
Stars eti kwa kuwa ilikuwa inakutana na Algeria kwa kuwa hatuwawezi.
Walisema mengi ikiwa ni pamoja na kusema kwa kuwa
hatujakuza vijana ni sawa na kukurupuka na kupita njia ya mkato. Kinachoelezwa
ni kitu kizuri, lakini kililetwa katika kipindi ambacho si sahihi Ratiba
tunacheza na Algeria, ilikuwa wazi kwa miezi kadhaa.
Angalau wangeza kushauri mapema, waliacha kila
mechi ikapita ikiwemo dhidi ya Nigeria, mechi mbili za Malawi na hawakusema.
Algeria ndiyo ikawa shida kwa kuwa iliteuliwa kamati ambayo mwisho ilionekana
inaingilia maslahi yao binafsi, hapo ndiyo ikawa vita.
Ninaweza kuachana na sehemu hiyo na kuiweka
kiporo kutokana na hali halisi ya baadaye. Ninaweza kuelezea mengi zaidi ya
hapo ambayo baadhi nina ushahidi nao wa maandishi kama vile malipo kwa baadhi
ya waliolipwa katika mechi za nyuma kuitangaza mechi ya Taifa Stars, kamwe
hawakupiga kelele kwamba tunatakiwa kukuza vijana. Wakaanza kupiga kelele baada
ya kuona maslahi yao yamebanwa, hivyo hawakuwa wazalendo.
Acha niingie kwenye upande wa pili ambao
nilieleza ni kuhusiana na viongozi wengi wa TFF kwamba si watu wanaoupenda
mpira. Si wapenzi wa kweli wa maendeleo ya soka nchini na zaidi wako pale kwa
ajili ya kushibisha matumbo yao.
Nikiwa ndani ya kamati nilishangazwa na mambo
mengi sana. Nilianza kuamini kuwa yale ambayo nimekuwa nikiyaandika kwa miaka
sasa yana ukweli mwingi sana, ninapaswa kuendelea kuyasisitiza.
Mengi niliyoyajua yalinikatisha tamaa, lakini
nikapiga moyo konde na kusimama upya na ndiyo maana leo ninaandika makala haya,
ndani ya TFF, kuna lundo la uozo.
TFF ndiyo shirikisho kubwa lililojaza watu wengi
wenye uwezo mdogo wanaofanya kila kinachotakiwa kuwa bora na huenda wapo hapo
kwa kuwa wanajuana sana na uongozi wa juu, walimsaidia Jamal Malinzi kuingia
madarakani au vinginevyo.
Watu hao si wazalendo, wengi wao ni wale
wanaofaidika na safari au wanaoishi kwa kutegemea ahsante ya kuusaidia uongozi
kuingia madarakan, lakini kamwe hawana uwezo hata kidogo.
Nitaanza na anayeitwa mratibu wa Taifa Stars,
Bwana Chacha. Huyu bwana, hajawahi kuwa kiongozi wa juu wa timu yoyote ya
daraja la kwanza au Ligi Kuu Bara.
Sasa ndiye mratibu wa Taifa Stars, mtu ambaye
anafanya karibu kila kazi ya maandalizi ya kambi ya Taifa Stars ambayo iko
ndani na nje ya Tanzania.
Ndiye alisafiri kwenye kufanya maandalizi ya
kambi ya Afrika Kusini. Ndiye alisafiri kwenda kufanya maandalizi ya sehemu
itakapofikia Taifa Stars kule Algeria na kwangu ninasema yalikuwa ni makosa
makubwa.
Soka la sasa, pamoja na utaalamu, angalau uzoefu
pia unaweza kuwa chachu. Chacha si mzoefu, hana elimu ya masuala ya soka au si
mjuzi wa mipango lakini kila kitu kimewekwa kwake.
Kwangu namuona si mtu anayejua mambo mengi au
kumtanguliza kwenda kuandaa kambi ta Taifa Stars dhidi ya Waarabu ni kichekesho
kikubwa kabisa!
Chacha anakwenda kuandaa kambi wakati hajawahi
hata kuandaa kambi ya timu kama Stand United inayojiandaa kucheza na Yanga au
Simba? Ametokea wapi, kwa uzoefu upi na je, kweli anastahili kufanya kazi za
Taifa Stars?
Chacha analazimika kuuliza mambo lundo, Chacha ni
mgeni katika mambo anayoyafanya lakini ndiye anayefanya majukumu hayo makubwa.
Sasa nimeelezwa kuwa amepewa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano. Huu mpira
tunaupeleka wapi, sababu za kufikia nafasi hiyo si vigezo, badala yake ni kwa
kuwa ni rafiki mkubwa na mwaminifu kwa Malinzi!
Katika maisha yangu, sijawahi kusafiri na timu au
Taifa Stars bila ya kazi muhimu na maalum. Ninakwenda safari kwa kuwa ninaijua
kazi yangu, ninajua nitaifanya kwa ufasaha.
Sijawahi kusafiri na timu kwa ajili ya kwenda
kufanya manunuzi tu yangu, ya rafiki zangu na familia yangu kama ninavyoona
viongozi kama Chacha wanavyofanya. Kwangu nakuwa wazi, hana faida sahihi ya
kufanya kinachotakiwa na kuisaidia Stars lakini yuko hapo kwa sababu ya
uaminifu wake kwa Malinzi au ahsante kwa kiongozi huyo.
Haiwezi kuwa sahihi kiongozi au mtendaji wa TFF
awe pale kwa kuwa tu ni mwaminifu kwa mtu au kiongozi. Kwanza lazima awe bora
kiutendaji, awe mwaminifu na anayelipenda taifa lake na timu ya taifa,
mwaminifu kwa nchi na timu ya taifa na si kwa kiongozi.
Wako waliosema, inawezekana Bwana Chacha
anatumika vibaya. Mimi nikasisitiza, “Namjua kwa uadilifu, ni mtu mwema, tatizo
ninacholilia ni uwezo wake na nafasi anayopewa. Ndiyo maana tunaanguka halafu
tunasingizia hatujakuza vijana. Yako mengi yanayotushusha, moja wapo ni kuwa na
watu wenye uwezo mdogo au duni kulingana na nafasi walizopewa kishkaji.”
Kichekesho kingine ambacho nimekishuhudia ndani
ya hilo ni ufujaji tu wa fedha. Mfano, kamati ambayo ilikuwa inahusika na timu,
ilipanga mambo yawe hivi; timu iondoke na ndege ya kukodi ya Fastjet ambayo
wangepanda wachezaji, makocha, viongozi na mashabiki kwenda moja kwa moja
kupambana na Waalgeria.
Stars ilipanga kutoka Dar es Salaam, ingetua
jijini N’djamena, Chad ndege ‘ingekunywa’ mafuta, baada ya hapo ingeondoka
kwenda Marakech, Morocco. Hapo timu ingetulia hadi siku ya mechi, halafu
ingeruka dakika 45 kwenda kuwavaa Waalgeria, baada ya hapo ingeondoka kurudi
Tanzania.
Lengo lilikuwa ni kukwepa hujuma na fitna za
Waalgeria ambao ninaamini lazima ‘waliitekenya’ Taifa Stars kutokana na
ilivyoingia Algers kizembe kabisa.
Wakati kamati inashughulikia hilo la Fastjet,
tena likiwa katika hatua za mwisho kabisa na makubaliano yamefikiwa, ilipata
taarifa TFF ilikuwa imeshalipa tiketi za ndege kutumia Turkish Airways!
Hii ilileta mkanganyiko wa juu kabisa kati ya
kamati na TFF. Watu wa kamati walitoa taarifa kwa shirikisho wanachofanya
lakini TFF waliendelea kufanya bila ya kuzungumza lolote hadi walipofanikisha.
Mwanakamati mmoja aliyepambana kuwashawishi
Fastjet kupunguza bei kwa kiasi cha chini kabisa, alijikuta akimwaga chozi
kuhofia heshima yake kuvurugika.
Fastjet baada ya kupewa taarifa hiyo walikasirika
kabisa. Waliona ni uswahili wa hali ya juu na mwisho kuna gharama walizokuwa
wameingia wakataka walipwe haraka sana.
TFF haikuwa tayari kulipa, yule mjumbe hakuwa na
uwezo huo na alikwishavunjika nguvu. Hivyo Mwenyekiti wa Kamati, Faroukh
Baghoza akalazimika kutoa mfukoni mwake zaidi ya dola 1,000 (zaidi ya Sh
milioni 2.5) ili kufidia gharama.
ZAIDI ENDELEA KUSOMA SEHEMU YA NNE







0 COMMENTS:
Post a Comment