Na
Saleh Ally, Johannesburg
KIKOSI
cha Taifa Stars kipo kambini jijini Johannesburg kikijiandaa na mechi dhidi ya
Algeria kuwania kucheza Kombe la Dunia.
Mechi
hiyo itapigwa Novemba 14 jijini Dar es Salaam kabla ya kurudiana Novemba 17
ugenini Algeria.
Katika
kambi ya Stars, Mkongwe Abdallah ‘King Mputa’ Kibadeni ni mshauri wa masuala ya
ufundi wa Taifa Stars.
Gwiji
huyo wa ushambuliaji katika kikosi cha Simba na Taifa Stars. Amekuwa hapa tokea
mwanzo na anaona mambo yanakwenda vizuri na imani kwamba Algeria ni timu bora
lakini si kweli kwamba haifungiki.
Kibadeni
anasema Watanzania hawawezi kulala na kuwaacha Algeria wafanye wanavyotaka kwa
kuwa yeye amekutana nao mara kadhaa akiwa kocha, akiwa mchezaji na wamewahi
kufanya vizuri dhidi yao.
Championi:
Timu imefika salama Afrika Kusini. Nini hasa ambacho kimeanza kufanyika?
Kibadeni:
Timu imefika salama, walimu wa timu Mkwasa na Morocco wameanza kazi na wameanza
kuyafanyia kazi mapungufu.
Championi:
Mapungufu yapi hasa ambayo yameanza kufanyiwa kazi?
Kibadeni:
Umeona vijana wamekuwa wakifanya mazoezi ya nguvu kwa kuwa kocha aliona wengi
katika timu zao walipokuwa wakicheza ligi hawakuwa fiti kiasi cha kutosha.
Championi:
Unaizungumziaje Algeria ambayo Stars ina kibarua cha kuivaa Novemba 14 ambayo
si mbali?
Kibadeni:
Kweli ni wakubwa, kwenye viwango vya Fifa wako juu lakini hilo lisitupe tabu
kwa kuwa tuko chini basi tukate tamaa. Vijana wajitume na kila mmoja ajitume.
Timu
ya Tanzania si mwisho wa vijana wetu na wanaweza kuitumia mechi hiyo na ile ya
ugenini kuonekana.
Championi:
Umeshauri nini kuhusiana na suala la kutotulia. Maana wachezaji wa Stars
walionyesha kuwa na uoga katika mechi dhidi ya Nigeria na pia Malawi?
Kibadeni:
Kweli, hilo ni suala ambalo makocha wanalifanyia kazi. Suala la kubaki na
mipira na utulivu kila wanapofikia langoni. Haya ni masuala ambayo walimu
wanayafanyia kazi kuhakikisha kunakuwa na uhakika katika umiliki wa mipira pia
kutumia nafasi.
Ninaamini
walimu wakifanya kazi yao vizuri na vijana wakijituma, basi mafanikio
yatapatikana.
Championi:
Mazoezi makali katika kipindi hiki unaona ni sahihi kutokana na utaalamu wako?
Kibadeni:
Hakika ni sahihi, ilikuwa ni kupambana na hali ya hewa ya hapa ili tukirejea
nyumbani tuwe fiti. Mkwasa na Morocco walilenga kuhakikisha vijana wanakuwa
fiti katika kiwango sahihi na sawa na kuongeza uimara wa kujiamini.
Championi:
Kuna tofauti ya uchezaji wa Waarabu wa zamani wakati wa enzi zenu na hawa
wanaokutana nao vijana?
Kibadeni:
Hakuna tofauti kubwa, kweli wana nguvu na warefu. Lakini tumewajenga vijana
kuwa zile nguvu zao si za kuuwa watu ila kuna mbinu za kupambana nao.
Championi:
Wana mtindo wa kusaka sare ugenini na kumalizia nyumbani, unafikiri watabadili
hilo?
Kibadeni:
Hata ugenini wanaweza kufanya vizuri msipokuwa makini. Lakini vijana
tunawajenga na kuwaeleza matokeo mazuri nyumbani yatakuwa nguzo ya mechi ya
pili. Utaona matokeo mazuri ya nyumbani dhidi ya Malawi ndiyo yaliyotubeba.
Championi:
Waarabu wazuri wa mipira ya vichwa kwenye vichwa iwe kufunga au kuokoa,
mmelifanyia kazi?
Kibadeni:
Makocha wanaendelea kulifanyia kazi na kuna njia ya kudhibiti hali hiyo.
Championi:
Vipi kuhusu mipira ya adhabu ambayo Waarabu ni wazuri?
Kibadeni:
Hapo ni suala la umakini na ndiyo nililizungumzia. Makocha wanalifanyia kazi,
sisi pia tunaungana kuwakumbusha na kuhakikisha hatutoi nafasi hizo ambazo
wakiwa ugenini ndiyo wanazitafuta sana.
Championi:
Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta
hawajaripoti kutokana na majukumu. Ikitokea imeshindikana kama ni majeruhi au
wanaumwa, ingawa hatuombi. Je, mmejiandaa na hali hiyo?
Kibadeni:
Hakika hakuna anayeomba kama unavyosema. Lakini uwezo wa kupambana upo, katika
soka hauwezi kuwa na uhakika wa jambo. Lolote linaloweza kutokea.
Hapa
kambini Afrika Kusini kuna vijana zaidi ya 25. Tuna vijana wanaoweza kucheza
nafasi za Samatta na Ulimwengu.
Kweli
kama imetokea hivyo, ninaamini akina Maguri na wenzao, wanaweza kupambana
lakini wakiwepo, basi ni vizuri kwa kuwa tunawahitaji zaidi kutokana na uwezo
wao ambao unakuwa msaada kwa wengine.
Championi:
Wako Watanzania ambao kwa hisia wanaamini Tanzania haiwezi kuing’oa Algeria.
Unawaeleza nini hao kwa mifano?
Kibadeni:
Kweli Waarabu wametupa tabu kwa miaka mingi sana, ndiyo maana watu wanaingia
hofu na imekuwa mazoea kwamba hatuwawezi. Lakini ilifikia wakati taratibu
tukabadilika.
Simba
nakumbuka 1974 tulihangaishana sana na Mehara El Kubra na mwisho wakatutoa kwa
penalti. Hapo ndiyo tukaanza kuamini mambo yanawezekana.
Championi: Ukiwa Simba unafundisha, haukuwahi kukutana
na timu za Waarabu?
Kibadeni:
Ilitokea, walikuwa ni El Harash ya Algeria. Tulipambana nao tukawapiga bao 3-0.
Tukaenda kuweka kambi Ufaransa tukiwa na akina Jenerali Ulimwengu, Marehemu
Nnauye wote walikuwa pale, hii ilikuwa ni mwaka 1983.
Tulipoenda
kwao na fitina na wakatufunga 2-0 lakini tukawa tumewatoa. Hivyo Watanzania
wanapaswa kutuamini na kujitokeza kwa wingi uwanjani ili tuwavunje nguvu hao
Waarabu.
Championi:
Unafikiri bao za Dar es Salaam zilizowalinda wakati huo, ndiyo zinatakiwa
kutiliwa mkazo mchi ya Jumamosi?
Kibadeni:
Kufunga mabao mengi katika mechi ya nyumbani ni jambo muhimu sana. Pia tukiwa
kwao tujitahidi sana wasitufunge zaidi ya bao moja au wasifunge kabisa.
Championi:
Kambi kwa ujumla iko vipi?
Kibadeni:
Kambi ni nzuri sana, nawashukuru sana TFF kwa kututekelezea kila tunachohitaji.
Pia nawashukuru sana kamati ya Taifa Stars maana ni watu wanaojitolea wakiacha
shughuli zao. Nyie waandishi kuja hapa mnatupa moyo, pia Watanzania wote kwa ujumla.
Ninawaomba wakubali kuwa tunatakiwa kupambana hivyo waungane nasi kwa vile
Algeria hatuwezi kuwang’oa tukiwa tumelala au tukishakubali kwamba hatuwawezi.
MAKALA HAYA YALIYOTOKA LEO KATIKA GAZETI LA CHAMPIONI, TUMEITUPIA HAPA KWA WALE AMBAO HAWAKUPATA NAFASI YA KULISOMA GAZETI HILO AU WALE WANAOISHI NJE YA TANZANIA.
0 COMMENTS:
Post a Comment