Kocha wa Simba, Dylan Kerr ameondoka nchini kwenda Afrika Kusini huku akisisitiza kwamba anataka mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa atakayeweza kusaidiana na Hamisi Kiiza kuipa Simba mabao.
Kocha huyo
alikwea pipa jana Jumapili kwenda Sauz ikiwa ni safari binafsi lakini pia akiwa
huko atapata fursa ya kuangalia uwezekano wa kupata fowadi aliyemlilia tangu
mwanzoni mwa msimu huu, pamoja na beki wa kati atayesaidiana na Juuko Murshid
na Hassan Isihaka.
Katika ripoti
yake, Kerr alisema kuwa alipendekeza atafutiwe fowadi mmoja anayejua nyavu kwa
ajili ya kusaidiana na Hamisi Kiiza, ambaye amekuwa ndiye jicho tangu kuanza
kwa ligi kuu msimu huu akiwa na mabao nane.
Mratibu wa Simba,
Abbas Ally, amesema kuwa, kocha huyo anatarajia kurejea Bongo Jumapili ijayo,
tayari kuanza kwa mikakati ya kuikabili Azam katika mchezo wa Ligi Kuu Bara
utakaopigwa Desemba 12, mwaka huu.
“Ni kweli kocha
ameondoka leo (jana Jumapili) kwenda Sauz, anatarajia kurejea Jumapili wiki
ijayo ili kuendelea na majukumu yake ya kikazi. Timu inatarajia kuanza mazoezi
Novemba 16, kujiandaa na mchezo wetu dhidi ya Azam,” alisema Ally.
Ally hakutaka
kuweka wazi iwapo Kerr ataangalia mchezaji anayeweza kumsajili kutoka huko
lakini Championi Jumatatu linafahamu kuwa atakuwa akisaka straika pamoja na
beki.
Simba inatajwa
kumuwinda straika wa Vital’O, Laudit Mavugo lakini imetega macho yake sehemu
nyingi ili kuweza kupata straika sahihi wa kutatua tatizo lao la ushambuliaji.
0 COMMENTS:
Post a Comment