Na Saleh
Ally
KUMEKUWA
na mambo mengi sana yanazungumzwa kuhusiana na kikosi cha SImba kinachoshiriki
Ligi Kuu Bara na kwa hali ya ushabiki inaonekana kwamba hakina mwenendo mzuri.
Maneno
kutoka kwa mashabiki, baadhi ya viongozi na hata wachezaji wenyewe yamekuwa
yakisigana kuonyesha hakuna mwelekeo ambao ni sahihi.
Taarifa za
kwamba baadhi ya viongozi wameitenga timu hasa baada ya kipigo cha Yanga cha
mabao 2-0, baadaye ikaelezwa walifanya hivyo mara baada ya kipigo cha bao 1-0
kutoka kwa Prisons.
Kocha
Dylan Kerr alishatamka wazi kwamba anaona ni bora kuondoka zake kwa kuwa
mwenendo ndani ya kikosi haumfurahishi. Inawezekana ni woga wa ajira ndiyo
maana hakutaka kusema kila kitu wazi, lakini inaonekana kutakuwa na shida kati
yake dhidi ya uongozi.
Uchunguzi
wangu wa kawaida tu, tayari nimegundua ndani ya kikosi cha Simba kuna makundi
ambayo yanatokana na watu ambao wako ndani ya timu kama sehemu ya uwakilishi wa
baadhi ya viongozi.
Kwamba
ndani ya kikosi cha Simba, wao kazi yao kubwa ni kupeleka maelezo kwa baadhi ya
viongozi nini kimefanyika na kuchukua maelekezo nini kifanywe.
Baadhi ya
kazi za watu hao, baada ya kupeleka mrejesho ya walichokiona ndani ya timu,
hupewa maelekezo yakiwemo kama yale ya hivi; fulani acheze na fulani asicheze
na hapa sasa yanakuwa tena si matakwa ya kocha na badala yake, kiongozi fulani
anataka nini.
Najua,
Watanzania wengi hawapendi kukosolewa na wepesi sana kuukanusha ukweli kwa kuwa
hawaupendi lakini Simba inaweza kuwa na kocha bora, lakini baadhi ya viongozi
wakageuka tatizo na kuwaangusha wenzao.
Au
viongozi hao wanaweza kugeuka tatizo na kuiangusha Simba yote ambayo ndani yake
kuna juhudi ya watu wengi sana, hata wale tu wanaokaa jukwaani kuishangilia,
kumbuka hupoteza fedha zao, muda wao na nguvu wanazotumia kuipa morali timu yao
kwa kuishangilia.
Kumekuwa
na msigano mkubwa ndani ya kikosi cha Simba kama vile baadhi ya watu kutaka
kumuonyesha kazi Kerr na wako wanaofanya hivyo kwa kuwa hawaridhiki kitu lakini
kwa kuwa wana nguvu kutoka kwa viongozi au baadhi ya viongozi.
Ukiangalia,
tayari misimu mitatu Simba imekwenda bila ya kufanya vizuri ikiwa imeajiri na
kuacha makocha lundo ikiwezekana bila sababu ya msingi.
Huenda
kocha angeonekana mbaya sana kwa kuwa hakuwa tayari kumsikiliza kiongozi fulani
tena asiye rais wa klabu ya Simba. Badala yake ni mjumbe wa kamati ya utendaji
tu anayeamini anapaswa kusikilizwa.
Sasa ni
wakati mwingine Simba imeingia kwenye njia hiyo ya kuanza kuamini kwamba kocha
hafai kwa kuwa timu ilikuwa imecheza mechi 8 na kupoteza mbili. Jambo ambalo
kokote kule katika soka duniani, haliwezi kukubalika pia ni kichekesho cha
karne.
Uongozi
unajua, kwamba hata katika usajili wao kuna mengi ya kurekebisha. Uongozi
unajua wakati mwingine kutokana na matatizo ya kifedha kuna mahitaji kadhaa
walishindwa kufikisha kwa wakati mwafaka iwe kwa wachezaji au makocha lakini
wakavumiliwa.
Ajabu wao
kwa nini hawawezi kuvumilia hata kidogo? Vipi wakikosea wengine ionekane ni
tatizo kubwa sana wakati hata wao viongozi wanakosea na inaonekana si tatizo!
Rais wa
Simba, Evans Aveva, Ijumaa iliyopita alijitokeza mazoezini kwa kushitukiza. Si
jambo baya sana, kwa kuwa alitaka kuwaonyesha yuko makini na anajali lakini
hilo haliwezi kuwa jibu la kila tatizo la Simba, badala yake utimizaji wa
mahitaji ya kikosi.
Lakini
asisahau mambo mawili; hamasa kwa wachezaji kwa kuwa nao ni bindamu, hata kama
ni kuwasisitiza kujituma, kuna njia sahihi za kuzitumia. Pili; kusimama kwa
rais wa klabu na si kila mmoja awe na sauti kwenye kila kitu, jambo ambalo
haliwezi kuwa sahihi na litaiangusha Simba.
0 COMMENTS:
Post a Comment