Na Saleh Ally
MBWANA Ally Samatta amefunga bao muhimu kwa
kikosi cha Tout Puissant Mazembe na sasa inalazimika kupambana kwa hesabu
sahihi katika dakika 90 zilizobaki ili itawazwe kuwa bingwa wa Afrika kwa mara
ya tano.
TP
Mazembe inaamini ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Afrika kwa kuwa ina
kikosi imara ambacho kimejiandaa vyema kwa ajili ya kufanya wanalotaka.
Wakati wanataja ubora wa kikosi chao, wanajua
lazima wafunge mabao ili kufikia malengo na namba moja tegemeo katika hilo ni
Mbwana, kijana wa Kitanzania kutoka katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es
Salaam.
Samatta ni tegemeo la TP Mazembe na
amelionyesha hilo kwa kufunga bao muhimu dhidi ya USM Alger na timu yake
ikaibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye fainali ya kwanza.
Kiwango alichokionyesha Samatta kinaonyesha
mengi sana kwamba Tanzania kuna vipaji vingi na vimekuwa havichezi badala yake
‘vinachezewa’ ndiyo maana nchi hii imebaki kwenye dimbwi la “Kichwa cha
Mwendawazimu”.
Samatta ameanza kupanda baada ya kuonyesha
uwezo mkubwa akiwa na Timu ya Daraja la Kwanza ya Mbagala Market ambayo
ilipopanda tu ikanunuliwa na tajiri Mohammed Dewji, ikiwa Ligi Kuu Bara ikaanza
kutumia jina la African Lyon.
Samatta hakupata muda wa kuichezea timu hiyo,
akajiunga na Simba nayo alicheza nusu msimu tu. Alikaa zaidi ya miezi miwili
akiwa hajajiunga na Simba akidai kutekelezewa ahadi zake ikiwemo gari
aliloahidi atanunuliwa.
Nusu msimu ilikuwa tosha kwa TP Mazembe
kuamini Samatta anaweza. Tokea wamemsajili, kamwe hajawahi kuwaangusha na sasa
ni staa mkubwa Afrika ambaye amefikia kukataa kitita cha Sh bilioni mbili
kujiunga na Zamalek ya Misri ambayo inamtaka kwa udi na uvumba, hata leo hii.
Kidogo nikuhamishe, katika mechi ya juzi,
pia ulimuona Mtanzania mwingine, Thomas Ulimwengu ambaye alipambana vilivyo
kuhakikishaa anaisaidia Mazembe kushinda mechi hiyo dhidi ya USM Alger.
Samatta na Ulimwengu, Watanzania hawa vijana,
wanategemewa na klabu kubwa kama TP Mazembe kuisaidia timu yao kubeba ubingwa
wa Afrika na wanaonyesha wanaweza kwa kuwa wameifikisha fainali na wamefanikiwa
kuiongoza kushinda mechi moja ya fainali, imebaki moja wakamilishe kazi yao.
Swali langu, vipi Samatta na Ulimwengu
imeshindikana kutegemewa na Yanga, Simba au Azam FC kufanya hayo wanayoyafanya
sasa TP Mazembe?
Swali
tena, Ulimwengu ambaye hata Moro United tu walimuona hana uwezo wa kufanya
vema, vipi leo anakuwa tegemeo kwa TP Mazembe inayotarajia kutwaa ubingwa wa
Afrika?
Kuna kitu tunapaswa kujifunza mara nyingi
sana wakati tukiendelea kushangilia mafanikio ya Watanzania hao ambao
inaonyesha kuna wengi wako hapa nyumbani, lakini hawawezi kufanya vema, kuinuka
au kuutumia uwezo wao vema kwa kuwa wanakandamizwa, wanadharauliwa au viongozi
ndiyo wanaoendesha ‘shoo’ badala ya wachezaji.
Lazima tukubali kuna tatizo kubwa ndani ya
viongozi wetu wanaoongoza klabu nyingi za hapa nyumbani.
Nasisitiza, wapo wengi zaidi ya wale walio
waelewa na wanaolenga kuendeleza mchezo wa soka nchini.
Uwezo wa Samatta na Ulimwengu haujaanza
kuonekana DR Congo. Hapa haukupewa nafasi kwa kuwa viongozi kwenye klabu
wanajua hata kuliko makocha na ninaendelea kusisitiza kumekuwa na viongozi
wanawapangia timu makocha au kutaka wachezaji fulani wacheze kwa ajili ya
maslahi yao binafsi.
Kwa hali hiyo ilikuwa vigumu Ulimwengu
kuonekana anaweza zaidi ya maneno kwamba ni mchezaji wa nguvu tu hawezi kufika
mbali. Alipo hapo, wengi wanasikia aibu kwa kuwa walimdharau.
Lakini hata Samatta anaondoka kwenda
Mazembe, wapo walioamini baada ya muda mfupi atarejea lakini anazidi kupaa na
sasa maisha yanazidi kusonga kwa furaha zaidi.
Kwanza tuwapongeze Samatta na Ulimwengu kwa
kuonyesha inawezekana. Wameachana na Utanzania (tabia za kioga), wameamini nje
inawezekana, wametoka na leo wanafanya vema. Lakini pia tukubali, kuna watu
wengi kwenye mpira wamejazana kukwamisha vijana wanaotaka maendeleo na hii
inatokana na viongozi kuamini wanajua sana mpira kuliko makocha na hata
wachezaji wenyewe.
0 COMMENTS:
Post a Comment