![]() |
| DK TIBOROHA (KUSHOTO) AKIWA NA MSEMAJI WA TIMU HIYO, JERRY MURO |
Klabu ya Yanga imeamua kujisalimisha katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufuatia amshaamsha ya Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli kwa kuwasilisha taarifa za mishahara ya wachezaji pamoja na wafanyakazi wote ili kuweza kulipa kodi.
Hivi karibuni, TRA ilifunga akaunti ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kusababisha shughuli kadhaa za kisoka kusimama, jambo ambalo limezishtua klabu kubwa, hivyo kuanza kujisalimisha.
Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha, ameeleza: “Huo ni utaratibu unaotakiwa kufanywa na kila idara, kwa upande wetu tayari tumeshafikia makubaliano ya kusaini leseni za wachezaji na tupo katika mchakato wa kuhakikisha tunawasilisha TRA taarifa zetu za mishahara za kila mchezaji na wafanyakazi wote wa Yanga ili kuweza kukatwa kodi.
“Suala hili kwa sasa lipo kwa mhasibu wa klabu, analifanyia kazi na tumedhamiria ifikapo mwezi ujao tutaziwasilisha taarifa hizo na kuweza kuanza kufanyiwa kazi.
“Suala hili linahusisha wachezaji wetu wote wa ndani na wa kimataifa kwa ujumla ili kuendana hali ilivyo.”
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Azam FC, Idrissa Nassor, amefunguka kuwa wapo tayari kufanya chochote kile watakachoagizwa na TFF juu ya masuala ya kodi kwa kuwa suala hilo lipo kisheria na linatakiwa kutekelezwa.








0 COMMENTS:
Post a Comment