Na Saleh Ally
Baada ya Ligi Kuu Bara kurejea, Simba imecheza mechi mbili na kufanikiwa kupata pointi mbili.
Simba imecheza na Azam FC na kutoka sare ta mabao 2-2 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo, Simba ilianza kufungwa, ikasawazisha na baadaye kufunga bao la pili. Lakini dakika chache tu, safu yake ya ulinzi ikaruhusu bao la kusawazisha.
Ikasafiri kwenda Mwanza ambako ilikutana na Toto African iliyokuwa imetoka ugenini Songea ambako ilitoa kipigo cha paka mwizi kwa Majimaji kwa kuitandika kwa mabao 5-0.
Mechi hiyo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ilikuwa ni ya hovyo kabisa kutokana na muonekano kama vile mechi ya mchangani.
Huenda hata baadhi ya mechi za mchangani zina nafuu kubwa na kamwe hauwezi kuwalaumu wachezaji kwa kuwa walijitahidi sana kucheza kwa juhudi na maarifa.
Uwanja ulikuwa umechakaa ile mbaya kutokana na mvua kubwa iliyokuwa imenyesha. Mara kadhaa mpira ulinasa kwenye madimbwi na hakukuwa na nafasi nzuri ya kuonyesha soka la uhakika.
Hata hivyo, Simba walijitahidi kuonyesha uwezo na soka la kuvutia ingawa halikuwa na nafasi kutokana na hali halisi ya uwanja ilivyokuwa.
Simba ilipata bao zuri kupitia kwa Danny Lyanga ambaye alifunga bao linaloingia kwenye rekodi ya moja ya mabao bora kabisa katika Ligi Kuu Bara.
Huku watu wakiwa wameanza kutoka uwanjani wakidhani Simba imeshinda kwa bao 1-0. Toto African walisawazisha bao katika dakika za nyongeza au majeruhi.
Krosi kutoka kwa beki wa kushoto ilimfikia mshambuliaji wa Toto African akiwa katika nafasi nzuri ‘aliyopewa’ na mabeki wa Simba.
Nahodha wa Simba, Hassan Isihaka ambaye ni beki wanayemwamini sana Simba lakini ameshindwa kuthibitisha kwa kipindi sasa kwamba anapaswa kuwa beki wa kuaminika, aliruka na kuukosa mpira huo.
Mfungaji akafunga kwa ulaini na kuipoka Simba pointi mbili ambazo ingezijumlisha na ile moja, ingeondoka na tatu.
Mechi iliyopita, Simba ilisawazishiwa bao tena baada ya kuwa imefungwa bao la dakika ya kwanza tu!
Kocha Dylan Kerr anapaswa kujiuliza mara mbili kuhusiana na safi ya ulinzi ambayo imekuwa na makosa mengi yanayozuiliwa.
Ni aibu beki kushindwa kuruka kichwa au kuwa na timing ya kuukoa mpira unaokwenda katika lango lake tena dakika za nyongeza.
Naamini Kerr atakuwa anakumbuka makosa kibao ya Isihaka ambaye ni beki mchanga aliyetwikwa mzigo mzito wa kuwa nahodha wa Simba na imeonekana wazi unahodha huo hautendei haki.
Kuna kila sababu sasa aweke ushindani katika safu yake ya ulinzi. Makosa katika mpira yapo, lakini hapaswi kuwepo mchezaji anayeonekana maarufu kwa makosa huku timu ikiendelea kuangalia.
Kama inawezekana atoe nafasi kwa walinzi wengine ili kuwapa nafasi viongozi pia kuangalia kama hawana kabisa beki au vinginevyo.
Huu ni wakati mwafaka Kerr naye atoe nafasi kwa Mohammed Fakhi au mabeki wengine, ampumzishe Isihaka na ikiwezekana changamoto zinaweza kumkuza zaidi.
Isihaka si beki mbaya lakini utachekesha ukisema ni beki kisiki. Bado anahitaji kukua, hii maana yake anastahili kujifunza zaidi na kupata changamoto zaidi.
Simba iachane na kuwa sehemu ya kukuza kila kukicha inaumia na mwisho inaishia kumalizwa na inaowakuza.
Rekodi ya Simba inazidi kuyumba kwa kuwa kikosi chake pia hakika kiongozi anayeweza kukielekeza kikosi hicho cha kufanya ni kipi.
Ndiyo maana mara kadhaa nimepinga Isihaka kuwa nahodha Simba, jiuliza kwa uzoefu wake wa msimu mmoja anaweza vipi kuwaongoza wenzake.
Kuna kila sababu ya kuwaamini vijana, lakini bado kuna kila sababu ya kuamini kupoteza kila mara au kukosea kila mara pia ni maumivu kwa rekodi za klabu hasa kama Simba inayoonekana ni kubwa, lakini yenye kikosi kidogo.







Ni hasira za kufungwa lakini mwalimu bado hajakosea. Huwezi kumkuza mchezaji kwa kumuweka benchi bali kwa kumpa nafasi na ndio anakuza kiwango. Mchezaji akikosea halafu ukamuweka nje maana yake unamnyima kujiamini na hata angekuwa bora kiasi gani!!
ReplyDelete