Na Saleh Ally
MISIMU
mitatu mfululizo, Simba imekuwa katika kipindi kigumu ambacho huenda kinazidi
kuwafanya mashabiki na wanachama wengi wa klabu hiyo kuwa na maswali mengi
yasiyokuwa na majibu hata nusu yake.
Kuna mambo
mengi yanayofanya mashabiki hao wa Simba kuwa na maswali yasiyo na majibu,
lakini kinachoumiza zaidi ni kuona ile sifa ya ukali unaonekana na neno Simba,
haupo tena!
Nani
anaweza kucheza na Simba, aungurumapo Simba, mcheza nani? Safari hii inaonekana
hata akiunguruma, wachezaji lundo na wala hawana hofu hata kidogo, hii ni Simba
kweli?
Hilo ni
swali ambalo wanajiuliza Wanasimba wengi sana, lakini bado wanakuwa na
matumaini kwamba mambo yatawezekana kabisa kwa kuwa ukweli, Wanasimba
wanasifika kwa kuwa na uvumilifu, angalau.
Hakuna
ubishi kuwa hawatavumilia kwa miaka mingine mitatu ijayo kama hali itakuwa
hivi; kwamba Simba ina timu inayoshindwa kushika hata nafasi ya pili kwa misimu
mitatu sasa.
Siti ya
Simba, imekaliwa na Azam FC, maana isipokuwa bingwa inashika nafasi ya pili.
Wanaobadilishana kileleni sasa wamekuwa Azam FC na Yanga.
Simba
inaendelea kupigania nafasi zinazofuatia ni maumivu kwa Wanasimba na huenda
wangefurahi msimu huu mambo yakabadilika na warejee katika nafasi hizo mbili
bila ya kujali ni ubingwa au nafasi ya pili.
Safu ya
ushambuliaji ya Simba msimu huu, imeendelea kuwa tatizo licha ya kwamba ndani
ya mechi 9 imefanikiwa kufunga mabao 15.
Utaona mabao 15 ni mengi, lakini Yanga iliyo
kileleni mechi sawa na Simba, ina mabao 20 na Azam FC katika nafasi ya pili ina
mabao 22. Tofauti ni mabao matano hadi saba ambayo si machache kwa ligi fupi
kama ya Tanzania.
Hivyo,
kweli Simba wanapaswa kuimarisha safu ya ushambuliaji na juhudi zimeanza baada
ya kuletwa kwa Paul Kiongera ambaye uongozi umeamua kumrejesha baada ya
kumpeleka kwa mkopo katika klabu yake ya zamani ya KCB ya Kenya.
Kwangu
ninaamini Kiongera ni mshambuliaji mzuri, hii naichukua kutokana na rekodi zake
za Kenya kuwa mmoja ya wanaofunga hadi mabao 15 kwa msimu. Hata alipoitumikia
Simba katika mechi chache kabla ya kuanza kwa msimu, alionyesha ana uwezo mzuri
kusaidia mashambulizi.
Kiongera
amerejea Simba, wanachotaka Simba ni kuona anaisaidia kupata mabao zaidi
yanayosaidia kupatikana kwa pointi. Lakini kama naye hatasaidiwa itakuwa ni
kazi bure, mwisho ataonekana hafai.
Lazima
tukubali, hakuna mchezaji anayeweza kufanya vema bila ya msaada wa wenzake.
Hivyo, wachezaji walio ndani ya Simba nao lazima wakubali kumpokea Kiongera,
kushirikiana naye na kuifikisha timu katika lengo sahihi wanalotaka uongozi na
Wanasimba wengine.
Kiongera
kwa kiwango cha ligi zetu kama hii ya Tanzania Bara, ana uwezo mkubwa wa kuwa
msaada sahihi kwa Simba hasa kama hataumia. Bado anaweza kukwamishwa kwa mengi
kwa kuwa ndani ya timu kuna mengi sana.
Najua
wengi wanahofia kusema ukweli, lakini wivu na husda pia ni matatizo makubwa na
yanawakwamisha wengi. Watakaofanya hivyo wajue hawatakuwa wameukwamisha uongozi
pekee.
Badala
yake watamkwamisha kweli Kiongera, watamkwamisha Rais wa Simba, Evans Aveva na
viongozi wengine, watawakwamisha mashabiki lakini mwisho watakuwa
wamejikwamisha wao kuchezea timu isiyokuwa na hatua.
Lazima
wachezaji walio ndani ya Simba wakubali pia kuwa pamoja na wakubaliane na mfumo
wa kusaidiana kama kitu kimoja.
Hakuna
timu iliyowahi kufanikiwa bila ya upendo. Hakuna upendo, mafanikio yanabaki
hadithi. Mpokeeni Kiongera lakini lazima mtangulize upendo na kuaminiana, ndiyo
mtaweza kuitoa Simba ilipo sasa.
0 COMMENTS:
Post a Comment