December 4, 2015

KIONGERA

Na Saleh Ally
NCHI yangu inaitwa Tanzania, watu wake wanaitwa Watanzania. Watu wenye maneno mengiii lakini vitendo ni tatizo kubwa kwao.


Ukitaka uonekane ni tofauti na Watanzania wengi wengine, basi kikubwa kuwa mtendaji au makini, mkali katika utendaji. Utasikia taarifa za kwamba unajidai sana au wewe ni kiherehere.

Watanzania wanapenda kuwa na muda mwingi wa kupumzika kuliko ule wa kufanyakazi. Kama hulijui hilo, angalia popote ulipo, baada ya saa, siku wiki au siku 14 utakuwa umejua hali ilivyo.

Sisi Watanzania wengi hatupendi kujituma, hatupendi kuhangaika au kufikiria sana. Badala yake vitu rahisi ‘vinavyoteleza’ tu ndiyo chaguo letu namba moja.
Mimi nimekuwa nikikerwa sana na kelele za usajili wa timu mbalimbali ambao zinatarajia kuufanya.

Kwa hapa nyumbani, karibu kila timu ya Ligi Kuu Bara imekuwa ikijipanga kufanya usajili mpya ili kujiimarisha katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.

Wakongwe Simba, tayari tumesikia wana mpango wa kumrejesha nchini Paul Kiongera, ambaye yuko kwao Kenya akikipiga katika timu ya KCB ambayo Simba imempeleka kwa mkopo.

Simba pia imekuwa ikimuwania mshambuliaji Laudit Mavugo, raia wa Burundi ambaye hata hivyo ameonekana kuwa kwenye ‘mikono’ mingi, maana hadithi ya kupatikana kwake sasa hadi imekinaisha.
OLUNGA
Kipindi hiki, kuna taarifa za kutaka kumpata mshambuliaji Michael Olunga raia wa Kenya ambaye sasa anakipiga Gor Mahia.
Ingawa Olunga mwenye ameishaweka wazi hajafanya mazungumzo na klabu yoyote ya Tanzania, lakini Simba inamuangalia kama mchezaji ambaye atakuwa msaada kwake kama atajiunga nayo.

Kweli safu ya ushambuliaji ya Simba inahitaji kuongezewa nguvu, lakini wakati wanahaha kuongeza mshambuliaji, utagundua jambo moja tu; hakuna anayezungumzia wachezaji wazalendo.

Simba hawataki kuzungumzia au kumfuatilia mchezaji yeyote wa ndani kwa kuwa wanaamini Tanzania ina tatizo la washambuliaji. Hivyo ni lazima kupata mshambuliaji kutoka nje ya Tanzania!

Mimi naona hili ni kama uvivu wa kufikiri tu, au kuamini vitu kwa mazoea ambalo si jambo jema. Simba wameamini nje ya mipaka ndiyo kuna wachezaji wazuri zaidi, lakini imefeli zaidi ya mara tatu kwa kuwasajili Simon Sserunkuma, Dan Sserunkuma na mbaya zaidi na inaudhi ni kumsajili Pape N’Daw kutoka Senegal.

Kweli kabisa ndani ya Tanzania washambuliaji hawapo, au wapo halafu hawaaminiwi kwa kuwa viongozi hawataki kusumbua akili zao na kufikiria.
MAVUGO

Makocha wa kigeni nao wameaminishwa kwamba Tanzania hakuna washambuliaji! Hivyo nao wanataka lazima mchezaji atoke nje. Akilipwa kwa dola, basi atakuwa na uwezo wa juu kuliko Mtanzania anayelipwa kwa shilingi?

Simba imefeli kwa wachezaji watatu niliowataja, lakini John Bocco na Elias Maguri wamecheza michuano ya Chalenji nchini Ethiopia na kufanikiwa kufunga mabao mengi zaidi ya Didier Kavumbagu, Amissi Tambwe wa Burundi pamoja na hata na Mavugo ambaye Simba inampigania.

Maguri aliyeonekana hafai Simba, anazidi kufunga akiwa Stand United, Taifa Stars na Kili Stars! Nafikiri kuna haja ya utafakari wa hili na ikiwezekana Simba wanaweza kubadili gia na kuangalia wachezaji wa hapa nyumbani.

Wachezaji wapo, washambuliaji bora kama Rashid Mandawa, Paul Nonga na wengine wanaweza kufanya vizuri kama wakiaminiwa tu. Maguri alionekana hafai, kaenda Stand, ameaminiwa na anafanya vizuri.

Hii ya kuamini kila mshambuliaji wa kigeni ndiye bora hata kama hafanyi vizuri nafikiri sasa inapaswa kuondoka kwenye vichwa vyetu na watu tuache uvivu wa kufikiri pia kutenda.

Muwaamini Watanzania wenzenu, kama ikishindikana au wasipofanya vizuri kutakuwa na cha kujifunza na kupita katika njia sahihi. Wageni wameiangusha Simba, waliwahi kuiangusha Yanga, waliiangusha Azam FC. Sasa vipi wageni tuliwapa nafasi na kwa Watanzania ionekane ni shida.

Lazima tukubali, hakuna tofauti kubwa kati ya wachezaji wetu. Tumekuwa tukitoa nafasi ndogo au mishahara midogo kwa wachezaji wa nyumbani. Waonyesheni thamani, wapeni nguvu nao watabadilika.


Kama hamtafanya hivyo, mtaendelea kutegemea wachezaji wa nje hata kama wana kiwango kidogo au duni ukilinganisha na wenyeji kama ilivyokuwa kwa N’daw ambaye nilimfananisha na muigizaji katikati ya uwanja.

2 COMMENTS:

  1. Klabu ya Simba msimu msimu huu inawajaribu washambuliaji wawaili wapya wa Kitanzania akiwamo Hija Ugandu na Dan Lyanga na hata jana wamechezeshwa, sidhani kwamba lazima imsajili Maguri au Boco ndio ionekane inawaamini Watanzania . Lakini pia si lazima wachezaji unaowaona wewe ndio wasajiliwe. Nonga na Mandawa hata timu ya taifa au Kili Stars hawakuitwa wala hukulalamika wewe wala mtu yeyote hadi tumepokea saba. Unataka Simba iwachukue wakati Yanga wamesajili Ngoma Azam wana Kipre, Simba unataka wawe na Mandawa kweli uko serious Simba igombee ubingwa na hao. Kila moja ya hizo timu 3 inahitaji kilicho bora ili kuleta ushindani na kufanya ligi yetu iwe bora zaidi,alamsik

    ReplyDelete
  2. Simba kuna UMBWE LA UONGOZI! Always hawajui nini wanataka na hawajui kusimamia wanachokiamua. Hii ndio maana kila siku kuna habari mpya ya usajili Simba, lkn mwisho wa siku hakuna anayesajiliwa. Nashawishika kuamini ni michezo ya kucheza na AKILI za wanasimba (MIND GAMES) ili wajue kuna kitu kinafanyika lkn mwisho wa siku sifuri!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic