December 28, 2015


Na Saleh Ally
UNAPOZUNGUMZIA mafanikio katika michezo kwa mtu mmojammoja hapa nchini, basi hakuna ubishi kwamba mshambuliaji Mbwana Ally Samatta ndiye aliyefanikiwa zaidi.

Samatta ambaye alichipukia akicheza soka katika vitongoji vya Kusini Magharibi mwa Jiji la Dar es Salaam, sasa ndiye mshambuliaji mwenye mafanikio zaidi barani Afrika.

Kama utazungumzia kwa miaka miwili, yaani 2014 na 2015, Samatta ndiye mshambuliaji aliyepata mafanikio makubwa zaidi kuzidi mwingine yeyote barani Afrika.

Samatta amefanikiwa na timu yake ya TP Mazembe kubeba ubingwa wa Afrika dhidi ya timu ngumu ya USM Alger ya Algeria tena akifunga bao katika mechi zote mbili za fainali, nyumbani na ugenini.

 Katika mechi zote mbili za fainali, TP Mazembe ilishinda kwa mabao 2-1 ugenini na 2-0 nyumbani, Samatta akawa mfungaji bora wa fainali, pia mfungaji bora wa michuano hiyo.

Sasa yuko katika fainali ya kuwania tuzo za Caf au Mchezaji Bora Afrika kwa wale wanaocheza ndani ya bara hili.

Samatta ni Mtanzania, anatokea katika nchi ambayo inaonekana imekwama kabisa kupiga hatua kimichezo tena na inaonekana afadhali ya zamani au enzi zile kuliko sasa.


Samatta sasa yuko katika hatua za mwisho kukamilisha suala la kuhamia Genk ya Ubelgiji na hatakwenda kufanya majaribio, badala yake ananunuliwa moja kwa moja.

Mshambuliaji huyo ni gumzo, pia yeye na mshikaji wake, Thomas Ulimwengu wamefikia kucheza hadi Kombe la Dunia la Klabu huko Japan, wiki chache zilizopita. Nini hasa wamefanya?
Samatta amekuwa juu zaidi, gumzo na ameendelea kufanikiwa, nini tofauti yake na Watanzania wengine ambao wameshindwa kuinuka? Au alifanya kitu gani hasa?

Lakini historia yake inaanzia alipokuwa akicheza soka la mchangani hadi baadaye kuisaidia Mbagala Market kupanda daraja kwenda Ligi Kuu Bara ibadilishwe jina na kuitwa African Lyon kabla ya yeye kuchukuliwa na Simba, hakukaa muda mrefu akajiunga TP Mazembe.

Katika mahojiano na SALEHJEMBE, Samatta ameeleza mambo kadhaa ambayo huenda hukuwahi kuyasikia.

SALEHJEMBE: Kwanza tuanze na jina lako, wengi wanachanganya kati ya Samata na Samatta, ipi ni sahihi?
Samatta: Kwangu sahihi ni Samatta, yenye double t. Kaka yangu ambaye yuko Mgambo (Mohammed) anatumia Samata, mimi niliamua kuitofautisha.

SALEHJEMBE: Safi, moja kwa moja twende sasa, hapa ulipofikia, kipi hasa umefanya na wengine wanashindwa au unawazidi nini ambacho wanapaswa kuchukua kwako?
Samatta: Kweli mimi naona sina tofauti kubwa na wengine, hakuna kikubwa nilichowazidi na hata uwezo wachezaji wengi wa Tanzania tunafanana sana.


SALEHJEMBE: Vipi wengi wanashindwa kutoka hadi hapo ulipo?
Samatta: Nafikiri ni mioyo, huenda wanatakiwa kubadili mambo kutoka kuwa na moyo wa Afrika Mashariki wawe na mioyo ya Afrika Magharibi.

 SALEHJEMBE: Unaweza kufafanua moyo wa Afrika Magharibi?
Samatta: Wenzetu wanaotokea katika nchi za Afrika Magharibi kama wakiamua kutafuta kitu fulani wakawa wanakipigania basi ni lazima wakipate. Watu wasichoke mapema, wapigane bila ya kujali kuna ugumu au vipi.

SALEHJEMBE: Ukiachana na kupigania, inaonekana wachezaji wengi wa Tanzania wanaweza kupambana, mafanikio kidogo wanalala, hauoni hili ni tatizo pia?
Samatta: Kweli, hilo ni tatizo kubwa. Hili sasa linakuwa ni upande wa thamani. Wengi hatuko tayari kuthamini kile unachokuwa unafanya kama kitu muhimu na unapaswa kukijali kuhakikisha hakiharibiki, pia si sahihi kuridhika mapema.

SALEHJEMBE: Kwani hadi umefikia hapo hauoni kama ni mafanikio makubwa na inatosha kabisa?
Samatta: Nina ndoto nyingi za kutimiza, niseme namshukuru Mungu, mfano ninachotaka ninapata kwa wakati kwa maana ya mahitaji. Lakini bado ninataka kupambana na changamoto mpya ili kwenda mbele. Sijaribidhika hata kidogo.


SALEHJEMBE: Ilikuwaje siku ya kwanza ulipopata taarifa kwamba TP Mazembe wanakuhitaji?
Samatta: Nakumbuka siku hiyo nilikuwa nyumbani, ilikuwa baada ya ligi na Ligi ya Mabingwa Afrika, sisi tulikuwa tumetolewa na hao TP Mazembe.

SALEHJEMBE: Taarifa ilikufikiaje?
Samatta: Alipiga simu Rage (mwenyekiti wa Simba wakati huo). Nilipopokea akaniambia kwamba TP Mazembe walikuwa wananitaka, alitaka kujua kama niko tayari.

SALEHJEMBE: Vipi ulimjibuje, ujifikirie kwanza?
Samatta: Hapana, kwanza nilijiamini hadi nikashangaa, nilimwambia wao wamalizane nao halafu baadaye wataniambia, akasema sawa atanipa taarifa.


SALEHJEMBE: Kutoka Simba kwenda TP Mazembe hakiwezi kuwa kitu kidogo. Hukuingia hofu hata kidogo?
Samatta: Nilianza kuona kama mbele kuna kiza, niliona ni jambo jipya, nikaanza kujiuliza maswali kadhaa. Usiku kidogo usingizi ulikata lakini nilijipa moyo ninaweza.
SALEHJEMBE: Mazingira ya Mazembe yalikuwa mapya kwako, vipi uliweza vipi kuingia na mwisho ukaweza?
Samatta: Kwenda katika mazingira yoyote mapya ukiwa mgeni ni changamoto kubwa sana. Kuna mambo mengi sana yanachanganya, mfano lugha, chakula na mambo mengi sana.

SALEHJEMBE: Hali hiyo huwasababisha wachezaji wengi wa Tanzania kutaka kurejea nyumbani. Vipi wewe ulivumilia?
Samatta: Nilikuwa ninataka kitu, ilikuwa ni lazima nivumilie. Lakini nilikuwa sijiamini kabisa mwanzoni.

SALEHJEMBE: Hujiamini kivipi?
Samatta: Unajua unatokea katika timu ndogo umejiunga na kubwa. Halafu unakuwa unaona kama kila kitu wanakudharau? Mfano wenyewe wanaweza kucheka tu mazoezini, unahisi wanakucheka wewe kumbe si hivyo.

SALEHJEMBE: Kuna kitu nafikiri kiliwashangaza watu wengi sana wakati unakwenda Mazembe, wakati ukiwa Uwanja wa Ndege wa Lubumbashi ulipokelewa na idadi kubwa sana ya watu na kama ungeshindwa kufanikiwa, huenda ingekuwa ni historia ya mchezaji aliyepokelewa mapokezi makubwa sana halafu akashindwa kuonyesha cheche?
Samatta: Hakika nilishangazwa sana na umati wa watu uliojitokeza kunipokea uwanja wa ndege. Maana ilikuwa utafikiri mchezaji mkubwa anayetua katika timu ndogo, idadi ile ilikuwa inashitua sana.

SALEHJEMBE: Unafikiri mashabiki hao walifurahishwa na nini kwao, taarifa kuhusu wewe ziliwafikiaje?
Samatta:…….

 Samatta ataelezea kuhusiana na hilo la mapokezi, lakini namna ilivyokuwa mechi yake ya kwanza na alivyoweza kupata namba katika kikosi cha kwanza cha Mazembe chenye nyota kibao kutoka kila sehemu barani Afrika.


USIKOSE MWENDELEZO WA MAKALA HAYA YA SAMATTA, KESHOKUTWA JUMATANO.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic