MBAMBA USWEGE (KATIKATI) AKISHUGHULIKIA UTOAJI WA TUZO ALIYOPOKEA MR II KUTOKA KWA JAKAYA KIKWETE AMBAYE WAKATI HUO ALIKUWA NI MMOJA WA MAWAZIRI KATIKA SERIKALI YA RAIS BENJAMIN MKAPA. |
Na
Saleh Ally
WAKATI
Mbamba Uswege akiwa katibu mkuu chini ya Simon Msofe, Chama cha Mpira wa Kikapu
Dar es Salaam (BD) kilikuwa kinajulikana na huenda umaarufu wake ulitokana na
gumzo la mchezo wa kikapu uliopatikana baada ya utendaji bora.
Licha
ya kuwepo kwa Mwenyekiti Msofe, lakini Uswege alikuwa maarufu sana kutokana na
kuwa mpiganaji kwelikweli.
Kipindi
cha Uswege, mambo mengi sana yalikuwa tofauti ukilinganisha na kipindi cha
miaka miwili baada ya kifo chake, halafu baada ya hapo ikawa si kupanda mlima
na badala yake kuteremka zaidi na zaidi.
Baada
ya kifo cha shujaa huyo wa mpira wa kikapu, leo hakuna chochote kipya ambacho
tasnia ya michezo upande wa mpira wa kikapu unapaswa kujivunia, nasema hakuna.
Kwani
viongozi waliofuatia baada ya Uswege wakaonekana hawakuwa na nia ya dhati, au
hawakuwa na mapenzi ya kweli kusaidia maendeleo.
Huenda
walifurahishwa na mafanikio ya Uswege ambaye alikuwa ushawishi mkubwa kusaidia
kupatikana kwa udhamini kutoka Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake
ya Kilimanjaro. Mpira wa kikapu, kila timu ilipata vifaa na wadhamini wakatoa
zawadi.
Changamoto
kwa maana ya ushindani ilikuwa kubwa, kulikuwa na Yanga na Simba ya mpira wa
kikapu ambayo ilizikutanisha timu za Pazi na Vijana. Ilikuwa ni mshikemshike
kwelikweli.
Lakini
kulikuwa na timu zilizojenga ushindani mkubwa kwa wakongwe Pazi na Vijana, kama
unawakumbuka ABC, JKT, UDSM, Don Bosco, Chang’ombe ambayo ilikuwa ina wachezaji
kama Mheshimiwa Temba ambaye sasa ni msanii maarufu wa muziki wa Hip Hop.
Raha
ya mpira wa kikapu haikushia katika timu, unamkumbuka Ramadhani Abdallah
‘Dullah’, Franklin Simkoko, Frank Bategeki, Michael Mwita, Ally Dibo na wengine
wengi walioufanya mchezo huo kuwa na mashamsham kila mechi zake
zinapochezwa. Sasa unamjua staa gani?
Upinzani
ulikuwa mkali hadi kufikia kuonekana umegawanyika mara mbili. Timu za jeshi
dhidi ya uraiani, pili timu za uraiani dhidi ya zile za uraiani.
Watu
walikuwa wakitokea sehemu mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam kwenda kushuhudia
mechi katika Uwanja wa Ndani wa Taifa.
Mpira
wa kikapu pia ulijumuisha michuano mbalimbali ikiwemo ile ya majiji ambayo
ilikuwa na ushindani wa juu kabisa na Dar, Mwanza na hata Mbeya baadaye
zilionyesha ushindani. Sasa kila kitu kinaonekana kimefeli na hadithi ni nyingi
kuliko vitendo.
Viongozi
waliongia madarakani baada ya kumpoteza Uswege, wengi walidhani mambo ni rahisi
kwa kuwa yalionekana yanakwenda poa kabisa. Kumbe hawakujua mtu huyo alikuwa
mchapakazi mwenye ndoto ya kuufikisha mbali mchezo wa kikapu.
Baada
ya mambo kuwashinda, watu hao zaidi walianza kulalamikia vyombo vya habari
haviwajali sana. Baadaye wakaelekeza lawama kwa wadhamini kwamba wameusahau
mchezo huo pia.
Kama
haitoshi kwa kuwa lawama zikawa ndiyo msingi, watu hao wakazidi kutupa lawama
zaidi na wakaziangusha kwa serikali kuwa imewasahau huku ikisaidia michezo
mingine. Nafikiri kulaumu kupindukia kuliwafanya wasahau kwamba serikali
haisadii michezo kabisa!
Wakati
wa Uswege hakulaumu waandishi wala wadhamini, badala yake alipambana na tatizo
kufanya mambo vema. Inaonekana walio kwenye uongozi wa vyama au klabu za mpira
wa kikapu ni watu wanaofaa kufanya kazi zinazohusu midomo pekee. Maana
wanazungumza tu na si watendaji.
Sasa
wana udhamini mzuri kutoka Azam, hata kama ungekuwa ni mdogo, lakini utaona
wana sababu nyingi za kufanikiwa. Wametengewa kipindi kwenye runinga, waandishi
bado wanawahoji, lakini bado wanalaumu tu na mafanikio hakuna.
Msiba
wa Uswege haukuwa wa familia yake tu, ni kwa Watanzania wote wapenda michezo. Leo
miaka 11 tangu msiba wake ulipotokea kwa ajali pale Makumbusho jijini Dar,
msiba unazidi kuwa mkubwa zaidi kwa kuwa juhudi zake zimeondoka, mpira wa
kikapu nao umeweka ‘pause’.
0 COMMENTS:
Post a Comment