Kuumia kwa mshambuliaji Donald Ngoma kumetengeneza nafasi kwa mshambuliaji Malimi Busungu ambaye anatarajiwa kupewa nafasi hiyo na Kocha Hans van Der Pluijm katika mchezo wa kesho dhidi ya Mgambo katika Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Ngoma aliumia bega katika mazoezi ya timu yake mapema wiki hii na anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa wiki kadhaa, kutokana na hali hiyo Busungu amesisitiza kuwa yupo tayari kwa kazi ili kuhakikisha Yanga inaibuka na ushindi katika mechi hiyo.
“Hivi karibuni kocha aliniita na kuniambia kuwa naweza kuwa mbadala wa Ngoma katika mechi hiyo kwa sababu ni majeruhi na inanibidi nipambane zaidi uwanjani.
“Nimejiandaa na nipo tayari kwa kila kitu, ninamuomba Mungu anijalie niweze kufanya vizuri kama ninavyotarajia licha ya kupata vitisho vingi kutoka kwa ndugu zangu wa Mgambo JKT ambao msimu uliopita tulikuwa wote katika kikosi hicho,” alisema Busungu.
Akizungumzia mchezo huo, Pluijm alisema: “Nimetengeneza kikosi changu kwa kutokuwepo mchezaji mmoja tegemeo na badala yake ninawaandaa wote, kama unavyoona Ngoma amepata majeraha, hivyo yupo Busungu na (Anthony) Mateo ambao wote wana nafasi ya kucheza.”







0 COMMENTS:
Post a Comment