SHIME AKITOA MAELEKEZO KWA WACHEZAJI WAKE WAKATI WAKIWA MAZOEZINI MJINI TANGA. |
Kocha wa Mgambo Shooting, Bakari Shime, ameibuka
na kutamba kuwa anatamani kupambana na wapinzani wake hata asubuhi
kutokana na maandalizi mazito waliyofanya.
Mgambo watakuwa wenyeji wa Yanga Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga wakati Ligi Kuu Bara itakapoanza kutimua vumbi tena.
Msimu uliopita, Yanga ilifanikiwa
kuvunja mwiko wa Mgambo kwa kuichapa mabao 2-0 katika Uwanja wa Mkwakwani baada
ya kusumbuana kwa muda mrefu na siku ya Jumamosi zitashuka kwenye uwanja huohuo
kusaka alama tatu.
Mgambo kwa sasa ipo nafasi ya tisa ikiwa
na alama 11 huku Yanga ikiwa nafasi ya pili na ina alama 23.
Shime alifunguka kuwa kwa sasa timu yao ipo vizuri, hivyo muda
wowote, hata iwe asubuhi wanatamani kupambana na Yanga na kuchukua pointi
zote.
“Safari hii Yanga haina nafasi kwetu kwa
jinsi tulivyojipanga natamani wafike hata leo na mechi yetu ichezwe asubuhi,
maana kusubiri mpaka jioni naona itakuwa kama tunapoteza muda kwa kweli.
“Na mchezo wetu tunaingia kwa kujiamini
kiukweli licha ya kutofanya usajili wowote dirisha hili lakini Yanga hawatupi
presha hata kidogo, zaidi tunafikiria kupambana tu na kuondoka na alama zetu
tatu.
“Nafahamu kuwa katika timu za Tanga sisi
walau tuko vizuri lakini tunataka kufanya vizuri zaidi kwa michezo yote iliyopo
mbele yetu ili kuhakikisha tunashinda yote,” alisema Shime.
0 COMMENTS:
Post a Comment