Uongozi wa Stand United, umetangaza
kuwa, klabu yoyote inayofanya mchakato wa kumsajili straika wao, Elias Maguri
kwa sasa inajisumbua kutokana na kwamba bado wanamuhitaji huku mkataba wake
ukitajwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.
Klabu kadhaa za ndani na nje ya Tanzania
zimekuwa zikihusishwa na kuihitaji saini ya kinara huyo wa mabao katika Ligi
Kuu Bara, ambaye msimu uliopita alikuwa akiitumikia Simba kabla ya kuachwa siku
za mwisho za usajili mwanzoni mwa msimu huu.
Timu ambazo zimekuwa zikihusishwa na
kuihitaji saini ya Maguri ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga na
mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, TP Mazembe ya DR Congo ambayo kesho
Alhamisi itaanza harakati zake za kuwania Kombe la Dunia la Klabu huko Japan.
Ofisa Habari wa Stand United, Deokaji
Makomba, amesema wamekuwa wakisikia taarifa za kutakiwa straika wao huyo lakini
hakuna hata timu moja iliyowafuata kuzungumza nao, lakini akatoa angalizo kuwa
hawapo tayari kumuachia kwa sasa kwani wanaihitaji huduma yake.
“Maguri bado ni mchezaji wetu na
ataendelea kuwa wetu mpaka pale mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu
huu.
“Tumesikia tetesi nyingi zikimhusu
Maguri kutakiwa na timu nyingi tu, lakini kati ya hizo hakuna hata moja
iliyokuja kuzungumza nasi kuhusiana na mchezaji huyo, lakini ieleweke tu hatupo
tayari kumuachia kwa sasa na hata kama mkataba wake ukimalizika na tukiona bado
tunamhitaji, tutakaa naye chini kujadili masuala ya mkataba mpya,” alisema
Makomba.
0 COMMENTS:
Post a Comment