December 17, 2015



Na Saleh Ally
Yanga imeifunga African Sports kwa bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, jana.

Mechi hiyo ilikuwa nzuri kwa maana ya kila timu kutaka kufunga na kushinda. Lakini uwanja uliharibu mengi maana hauko katika kiwango kizuri na huenda ni tatizo ambalo Bodi ya Ligi Tanzania inapaswa kuliangalia kwa jicho sahihi.

Ukirudi katika uchezaji, African Sports iliidhibiti Yanga hadi dakika za mwisho kabisa. Hakukuwa na tofauti kubwa ambayo ungeweza kuiona.

Kikosi cha zaidi ya Sh milioni 500 dhidi ya kikosi kilichoundwa kwa chini ya Sh milioni 100.

Soka liliendelea kuwa na ushindani hadi mwisho na utaona namna Yanga walivyoibuka na ushindi kwa makosa ya African Sports.

Kwanza ni mbinu duni za mwalimu, pili ni namna wachezaji walivyokuwa wameipania Yanga, wakacheza kwa gia moja tokea dakika ya kwanza hadi ya mwisho.

Mbinu kwa kocha; kweli hazikuwa sahihi, hakuonyesha kubadili njia sahihi na nini cha kufanya kama kujaza viungo na huenda kuiruhusu timu yake iuchezee mpira muda wote ili kujilinda.
Mfumo unasema hivi, mpira unapokuwa nao unakuwa tayari umejilinda. Adui au mpinzania analazimika kukukokonya kwanza kabla ya kushambulia maana yake hizo ni kazi mbili kwa wakati mmoja kwake.

Sports waliendelea kubutua kila wakati bila ya kujali kwamba Yanga walikuwa wana presha zaidi, hawakutaka kupata sare ya pili Tanga. Lakini wao Sports sare ingekuwa ushindi kwao, walipaswa ku relax zaidi.

Ajabu zaidi, kocha akakubali mfumo uleule wa kijinga wa miaka nenda rudi kupoteza muda kwa kujiangusha.

Mwisho wakafungwa bao dakika au sekunde 30 za mwisho kabisa za mchezo na hakuna ubishi walijiponza.

Kwa wachezaji; pia walipaswa kuwa msaada kwa kocha. Kwamba wamikamata Yanga kwa dakika zote lakini wakashindwa kwa sekunde 30. Kitu ambacho ni kuonyesha kiasi gani wachezaji wengi wa timu ndogo wamekuwa wakicheza kwa kukamia kupindukia kila wanapokutana na timu kubwa.

Kukamia si sehemu ya kufanya vema. Kukamia ni asili ya sifa, humfanya aliyekamia kuondoka katika hali yake ya kawaida inayoweza kutengeneza ufikiri sahihi wa kile anachokifanya kulingana na muda au hali halisi.

Unaweza kufanya vizuri kwa kutanguliza utulivu wa ufikiri, halafu ukaongeza na juhudi ambayo haifikii kukamia. Mwisho utafanya vizuri.
Utulivu wa dakika mbili za mwisho ulitosha kuikomboa Sports. Lakini kwa kuwa wachezaji waliamini kubutua na kujiangusha ndiyo jambo sahihi la kuwasaidia kupata sare, mwisho wakaanguka.
Kocha na wachezaji wa African Sports hawana sababu ya kulaumu au hawana wa kumlaumu. Wao ndiyo tatizo na ndiyo waliojimaliza.

Utaona bao la Thabani Kamusoko lina mambo mawili ambayo waliyakosa wao. Moja, Yanga waliendelea kupanga mipango sahihi hadi dakika ya mwisho wakiwa hawajakata tamaa kwa kuwa walitaka kutimiza walichokuwa wamekifuata.


Lakini utulivu wenye utimilifu wa malengo ya kufikia walichokitaka kwa Haji Mwinyi aliyepiga krosi, Donald Ngoma aliyetoa pasi ya kichwa na mfuyngaji Kamusoko ndiyo ungekuwa msaada kwa Sports.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic