December 14, 2015

BOSSOU

Na Saleh Ally
DIRISHA la usajili limekuwa na vituko vingi sana, huenda ndiyo wakati mwafaka wa watu wengi kupata riziki.

Riziki ambazo zimekuwa zikipatikana katika madirisha ya usajili ya ligi nyingi, zimekuwa ni zile zenye walakini kwa kuwa wako watu wengi wanaotaka kujifaidisha kupitia mchezo wa soka bila ya kujali wataufaidisha au kuuendeleza vipi.

Katika suala la usajili, kama binadamu kuna jambo la kukosea, kwamba sehemu fulani watu ‘wamebugi’, lakini sehemu kubwa ya usajili unaofanyika hapa nchini unaonyesha wazi kuwa ni upigaji ambao una mtandao mkubwa.
SHERMAN

Upigaji huo, hakika unaonekana hauna msaada mkubwa na soka ya Tanzania na wako wanaofaidika, ukianzia wakala, viongozi wa klabu na hata waandishi ambao hutumika kusifia wachezaji wakiwemo wale wabovu kabisa ambao mtu halazimiki kuvaa miwani au kusomea ukocha ili kuthibitisha kwamba hawana lolote.

Wakala Gibby Kalule ni kati ya watu ambao ninaamini anataka kuifanya Tanzania ni shamba la bibi kwa kuleta kila mchezaji aliyechoka kuja kucheza nchini na inaonekana Yanga ndiyo imekuwa sehemu yake mambo yanaweza kufanyika kwa ulaini, yakafanikiwa.

KAMARA

Kalule amekuwa mjanja na inaonekana anawazidi ujanja makocha na viongozi wa Yanga ingawa nachelea kusema wako ambao watakuwa wakishirikiana naye kukubali kufanya usajili ambao ni hovyo kabisa na hauna tija kwa Yanga wala soka hapa nchini.

Lengo si kulaumu, lakini nitatoa mifano namna ambavyo wachezaji walioletwa na Kalule wamekuwa wakionekana si lolote, lakini bado ana nafasi ya kuwaleta tena halafu kuna chombo cha habari kikafanya kazi kubwa ya kuwasifia tena kwa juhudi kubwa bila ya kujali ni kushusha hadhi au kukiuka misingi ya uandishi ikiwa ni pamoja na kuwadanganya Wanayanga.

Najua, ikitokea chombo kimoja cha habari kimeboronga, wasomaji mara nyingi hutupa lawama kwa kila chombo cha habari.

Kalule alimleta mshambuliaji Leonel Saint-Preux akajiunga na Azam FC, hakufanya vizuri sana ingawa alikuwa maji kupwa maji kujaa. Mwisho wake alikimbia na Azam wakaamua kuachana naye.

Nilianza kupata hofu baada ya kusikia kuna mshambuliaji anaitwa Kpah Sherman ambaye ameamua kuondoka Cyprus na kujiunga Yanga. Kiasi fulani nilianza kusema kuna tatizo lakini nimekuwa na kawaida ya kusubiri, mwisho wa mshambuliaji huyo raia wa Liberia kila mtu aliuona.

Alifanikiwa kucheza vizuri zaidi mechi moja tu ya Nani Mtani Jembe wakati Yanga ikipoteza kwa Simba. Yanga walikimbia mbio kumsajili. Baada ya hapo hadi anaondoka kwenda Afrika Kusini, hovyo kabisa.

Kama Yanga ilimuuza Sherman, huenda ilikuwa bahati sana kwao lakini ukizungumzia kwa ushambuliaji, nafasi alipewa kubwa ya kujaribu tena lakini alishindwa. Hakuna anayeweza kuniambia Tanzania hakuna washambuliaji wa aina ya Sherman.

Kiungo Lansana Kamara ambaye juhudi za Kalule kumuingiza Yanga zilikwama kabisa. Sijui kwa nini hapo awali benchi la ufundi la Yanga au uongozi haukuwa ukishtuka kama ulivyofanya kwa kiungo huyo.

Najua Kocha Hans van der Pluijm ndiye alikuwa kizingiti katika hilo. Mwisho katika mechi ya kirafiki Yanga ikicheza na SC Villa, kwa kuwa Kalule ni raia wa Uganda, alimsaidia Kamara kupata nafasi aonyeshe uwezo wake, aliishia kuwashangaza wengi na jibu lilikuwa ni “mchezaji wa kawaida kabisa”.

Baada ya hapo, filamu iliyofuatia ni ya Vincent Bossou, kawaida nimekuwa nikisema ni mchezaji aliyesajili Yanga kupitia picha ya Didier Drogba.

Picha hiyo wakati Bossou akiwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Togo, alikabana na Drogba, basi hiyo ikazungushwa mitandao yote kuonyesha Yanga inapata mtu kweli.

Ukiamua kutafuta picha za Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani wakikabana na Drogba, Kaka, Robinho, Samuel Eto’o ziko nyingi sana. Kila mmoja aliona, hata baada ya kusajiliwa, benchi la ufundi la Yanga lililazimika kuanza kumtengeneza Bossou kwa nguvu kubwa.

Hakupata nafasi ya kucheza hadi Cannavaro alipoumia au Yondani kutakiwa kupumzika. Usajili wa mchezaji mwingine wa mchezaji wa kimataifa aliyetakiwa kubaki benchi.

Kama unakumbuka, Kalule aliwapelekea Simba mshambuliaji kutoka Ghana aitwaye, Nelson Aboagye, fasta wakamshitukia na ‘kumtolea mbavuni’. Huko hakurudi, nguvu kaielekeza Yanga ambako kwake mambo ni utelezi tu.

Kalule ni mfanyabiashara, kwa faida ya maisha yake huenda akawa hatendi dhambi na ndiyo maana safari hii ameibuka na filamu mpya ya Issofou Boubacar ‘Diego’ ambaye sasa Yanga inamuangalia.

Mchezaji huyo ukiangalia rekodi zake hakika ni za kubabaisha sana mtandaoni. Hazionyeshi amecheza mechi ngapi katika timu au kufunga mabao mangapi. Video za mechi zake ndiyo zinachekesha kabisa.

Swali kwamba kweli huyo Diego tunayeambiwa alicheza Esperance ya Tunisia kweli anaweza kuwa mchezaji wa kuwaweka benchi watu kama Amissi Tambwe au Donald Ngoma?

Najua kwa wachezaji wazalendo wamekuwa wakionewa kwa kuwekwa benchi ili wageni nao wacheze au bosi anayetoa fedha asione ‘amepigwa’, lakini kama utalinganisha uwezo wa mgeni anayecheza na mwenyeji, unaona mwenyeji ndiye bora zaidi.

Yanga ina wachezaji wa kigeni kibao kama Tambwe, Ngoma, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima wanaofanya vizuri na hawa wote hawakuletwa na Kalule.
KALULE (WA PILI KUSHOTO) AKIJADILI JAMBO PAMOJA NA KOCHA MKUU WA YANGA, HANS VAN DER PLUJM, COUTINHO NA WACHEZAJI WAWILI WALIO CHINI YAKE, SHERMA RAIA WA LIBERIA NA KAMARA.

Wachezaji wa wakala huyo wanaonekana wazi wamekuwa si wa uhakika. Benchi la ufundi la Yanga linalazimika kufanya kazi ya ziada kuinua viwango vyao na wakati mwingi kuwaweka benchi wazalendo wenye uwezo ili mradi na wageni nao wacheze ‘kwa huruma’.

Hili si jambo sawa, Yanga lazima wafungue macho kuhusiana na mwenendo huu. Hizi habari za mipangomipango ikiwemo vyombo vya habari kuingia kwenye kusifia mchezaji kwa picha ya Drogba tu au hajacheza hata mechi moja tu si sawa.

Suala la kulifanyia kazi lazima liwe muhimu, likiendelea huenda nikalazimika kufanya uchunguzi wa ndani zaidi kama kuna kiongozi wa Klabu ya Yanga au ndani ya benchi la ufundi anayehusika na kinachofanyika sasa ambacho ni upotezaji wa fedha za klabu hiyo ya wananchi au dhuluma kwa wachezaji wetu wazalendo.


Kwani wageni hao na wakala wao wanalipwa mamilioni wakati wa usajili pia mishahara minono huku wakiwa benchi. Hili halikubaliki, nitarudi. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic