MTIBWA SUGAR |
Azam FC imeponea chupuchupu mikononi mwa Mtibwa Sugar baada ya kulazimisha sare ya bao 1-1 katika mechi ya Kombe la Mapinduzi kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, leo.
Mtibwa Sujgar ndiyo ilitawala sehemu ya mchezo kwa kiasi kikubwa huku ikipoteza nafasi nyingi za kufunga. Timu hizo zilikwenda mapumziko bila ya bao.
Azam FC ilionekana kuamka katika kipindi cha pili, lakini dakika tano tu za mwanzo na baada ya hapo, Mtibwa Sugar wakashika usukani tena hadi walipopata bao kupitia kwa Hussein Javu baada ya beki Said Morad kufanya makosa na mpira kumfikia Ramadhani Kichuya aliyempa mpira mfungaji.
Mtibwa Sugar wangeweza kupata mabao zaidi, lakini wakapoteza nafasi zaidi hadi Azam FC waliposawazisha bao kupitia kwa nahodha wake, John Bocco.
Bocco alifunga bao hilo kwa mkwaju wa penalti, dakika chache tu baada ya kuingia na kuangushwa wakati akiwachambua mabeki wa Mtibwa Sugar.
Kichuya aliinfungia Mtibwa Sugar bao safi katika dakika ya 88 akiunganisha krosi safi ya Baba Ubaya, lakini wakati mwamuzi akijiandaa kuweka mpira kati, mwamuzi msaidizi ambaye ni mwanamama, akasema mfungaji aliotea jambo ambalo lilizuia taharuki.
0 COMMENTS:
Post a Comment