Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeweka wazi kuwa nia yao kubwa ni kuziona timu za madaraja ya chini zinafanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho hadi kuwa mabingwa.
Bingwa wa kombe hilo ndiye ataiwakilisha nchi katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na bingwa wa ligi kuu atashiriki Klabu Bingwa Afrika, kwa maana hiyo timu za ligi kuu ikiwemo Simba, Yanga na Azam zitatakiwa kufanya kazi ya ziada kama zinataka kucheza kimataifa mwakani.
Kombe hilo ambalo linashirikisha timu zote za Ligi Daraja la Pili, la kwanza na ligi kuu, kwa sasa lipo raundi ya tatu ambapo itashirikisha timu za ligi kuu pamoja na zile zilizopenya raundi ya kwanza na ya pili.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema kuwa nia yao ni kuziona timu za madaraja ya chini zinafika mbali hivyo wamepanga timu hizo zikutane zenyewe kwa zenyewe ili kuzipa nafasi mojawapo kusonga mbele.
“Hatua inayofuata tutahakikisha timu hizi ndogo tunazipanga zicheze zenyewe kwa zenyewe ili japo tuipate timu moja itakayosonga hatua inayofuata, hivyo inaweza pia timu kubwa zikakutana na hapo moja lazima itatoka, tumeona timu hizi zina uwezo mkubwa zaidi ya zile za ligi kuu.
“Tumejipanga vizuri kama timu ikawa bingwa na haina uwezo wa kwenda kushiriki kimataifa TFF tutahakikisha tunaisaidia mwanzo hadi mwisho,” alisema Malinzi.
0 COMMENTS:
Post a Comment