Baada ya kikosi cha Simba kuonekana kusuasua katika michezo yake ya Ligi Kuu Bara, uongozi wa klabu hiyo, jana, Jumapili ulikutana na wazee wa klabu hiyo kwa lengo la kujadili mambo muhimu kuhusu timu yao ikiwemo mwenendo wa timu.
Simba ambayo leo Jumatatu itacheza mechi yake ya kwanza ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Jamhuri ya Zanzibar, katika michezo minne ya mwisho kwenye ligi imeambulia pointi sita, hali iliyoanza kuwatia wasiwasi Wanasimba juu ya kiwango cha timu yao.
Rais wa Simba, Evans Aveva, amesema kuwa, kikao hicho si kigeni kwani ni utaratibu wao kukutana na wazee wa klabu hiyo mara kwa mara.
Alisema kuwa wamejadili mambo mbalimbali na ya msingi ambayo hakuwa tayari kuyaweka wazi, lakini kikubwa ni kwamba wamekubaliana kuwa na umoja na ushirikiano ambao utaifanya timu yao ifanye vizuri katika Kombe la Mapinduzi na ligi kuu mara tu itakapoendelea.
"Tumefanya kikao cha kawaida na wazee wetu, tumewapa taarifa na kujua nini cha kufanya katika timu yetu ya Simba.
"Ni mengi tumeongea lakini kikubwa tumekubaliana kushirikiana na kuipa nguvu timu yetu iwe kufanya vizuri katika Kombe la Mapinduzi pamoja na ligi, wazee wametoa maoni yao na tutayafanyia kazi ili yalete faida kwa klabu," alisema Aveva.
0 COMMENTS:
Post a Comment