MANYIKA... |
Kocha Mkuu wa Simba, Muingereza, Dylan Kerr, amesema katika harakati zake za kuutetea ubingwa wa Kombe la Mapinduzi hatamtumia kipa wake, Muivory Coast, Vincent Angban.
Angban kwa siku za hivi karibuni ameonekana kukaa langoni katika kila mchezo wa Simba kwenye Ligi Kuu Bara kitendo ambacho kimemfanya kocha huyo kumpumzisha na badala yake kuwatumia Peter Manyika na David Kissu.
Katika michuano hiyo ambayo msimu uliopita Simba ikiwa chini ya Mserbia, Goran Kopunovic iliutwaa ubingwa huo, msimu huu Kerr amepanga kuwatumia zaidi wachezaji wasiokuwa na nafasi kikosini hapo akiwemo Novatus Lufunga, Mohammed Fakhi, Issa Said na wengine.
Kerr amesema Manyika amekuwa akionyesha kiwango cha roba mazoezini hali inayomfanya kumkabidhi mikoba yote ya Kombe la Mapinduzi akisaidiana na chipukizi, Kissu.
“Kiukweli Manyika amekuwa akijitahidi sana mazoezini, siku hadi siku naona kiwango chake kinakua, hivyo nimepanga kumtumia kwa muda wote kwenye michuano ya Mapinduzi akisaidiana na Kissu, kwa upande wa Angban yeye nitampumzisha.
“Michuano hii sijaitilia maanani sana kama ilivyo ligi kuu, lakini si kwamba naidharau, bali nitapambana kuhakikisha ubingwa wetu tunautetea, nawaamini vijana wangu, hawataniangusha,” alisema Kerr.
0 COMMENTS:
Post a Comment