January 11, 2016


Timu ya Azam ilifungashiwa virago katika michuano ya Kombe la Mapinduzi wiki iliyopita baada ya kushindwa kufanya vizuri katika mechi zake za hatua ya makundi.

Mpaka inaondolewa kwenye michuano hiyo, haikuwahi kushinda mechi yoyote zaidi ya kuambulia sare mbili huku ikipoteza mechi moja na kujikuta ikiburuza mkia kwenye kundi lake lililokuwa na timu nyingine za Yanga, Mtibwa na Mafunzo.

Hata hivyo mpaka kufikia jana Jumapili, Azam ndiyo inatajwa kuwa timu inayoongoza kwa utovu wa nidhamu katika michuano hiyo, hivyo kama kutakuwepo na tuzo ya nidhamu mbovu basi inaweza kwenda kwa kikosi hicho kinachofundishwa na Muingereza, Stewart Hall.

Pia Azam inashikilia rekodi ya kuwa na mchezaji aliyeonyeshwa kadi nyekundu katika michuano hii tangu ilipoanza kutimua vumbi Januari 3, mwaka huu.

Katika mechi yake dhidi ya Yanga, wachezaji wake watano walionyeshwa kadi za njano huku nahodha wake, John Bocco akionyeshwa nyekundu, rekodi ambayo haijafikiwa na timu yoyote mpaka sasa.


Kutokana na hali hiyo, mmoja wa waamuzi wanaochezesha michuano hiyo, Mfaume Ally, aliliambia gazeti hili kuwa hakuna timu nyingine ambayo wachezaji wake walipewa kadi nyingi za njao katika mechi moja kama Azam.

"Mashindano yanaendelea vizuri lakini kwa mtazamo wangu timu ya Azam ilishindwa kusonga mbele kutokana na mambo mengi lakini kubwa zaidi ni wachezaji wake kutozingatia sheria za soka kwani ndiyo waliongoza kupewa kadi katika mechi zote walizocheza," alisema Ally.


Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime, naye alisema: "Kama kungekuwa na tuzo ya utovu wa nidhamu basi Azam wangechukua tuzo hiyo kwani katika mechi zao zote walizocheza walionyesha utovu mkubwa wa nidhamu jambo ambalo siyo zuri kama wanataka mafanikio."

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic