MAYANJA (KULIA)... |
Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Jackson Mayanja, raia wa Uganda, amewapa majukumu mazito wachezaji wa timu hiyo wakiwemo wale wa kimataifa kuhakikisha wanabadilika na kujituma ili kuisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kudai kuwa uwezo upo iwapo wachezaji wataamua kujitoa.
Mayanja ambaye amekabidhiwa jukumu la kuinoa Simba baada ya kuondoka kwa Kocha Dylan Kerr, amejinadi kuwa Simba inao uwezo wa kutwaa ubingwa licha ya kuonekana haina uwezo huo kwa sasa. Kumbuka, kesho ina kibarua cha kuivaa Mtibwa Sugar.
Mayanja amefunguka kuwa anatambua jukumu alilopewa ni kubwa la kuiongoza timu hiyo lakini tayari ameshaanza mikakati ya kukifumua kikosi kwa nia njema ya kuwaandaa wachezaji kisaikolojia ambapo lengo lake kubwa ni kuona kila mmoja anacheza kwa uwezo wake wote ili lengo la kutwaa ubingwa litimie.
“Nataka kubadili akili za wachezaji kuhakikisha wanajitambua, pia kila mchezaji anatakiwa apiganie timu yake ili Simba iweze kuibuka na ushindi mwisho wa ligi.
“Mimi ni kocha wa kimataifa, nahitaji kuifikisha mbali timu yangu kwani nimekuja Simba kwa ajili ya kufanya kazi, wachezaji wa kimataifa nao wanatakiwa kutambua kuwa wanatakiwa kuonyesha uwezo wa juu zaidi kwa kuwa wanaangaliwa kwa jicho tofauti.
“Kama ni suala la ubingwa, timu bado inayo nafasi hiyo kwa kuwa nafasi yetu kwenye msimamo siyo mbaya, ila kwa kuwa katika mpira kuna mambo mengi lolote linaweza kutokea na kutakuwa hakuna jinsi ya kubadilisha matokeo ya Mungu,” alisema Mayanja.
0 COMMENTS:
Post a Comment