Na Saleh Ally
MSIMU wa 2003-2004 wakati Arsenal ilipocheza mechi za Ligi Kuu England na kufanikiwa kutwaa ubingwa bila ya kupoteza, Kocha Arsene Wenger alisema aliishi milele.
Wenger raia wa Ufaransa alisema ndiyo msimu pekee katika maisha yake aliishi milele kwa kuwa anaamini hakukuwa na presha kubwa zaidi ya moja ambayo ilimtangulia katika kila mechi, nayo aliishinda hadi mwisho wa msimu.
Presha hiyo ni “Kucheza mechi hii bila kupoteza”. Maana kila alipofika uwanjani alikuwa na hofu asipoteze na kuharibu rekodi, angalau alitamani ifikie mechi mia lakini mwisho wapinzani wao wakubwa Manchester United wakaharibu mambo.
Maelezo ya jumla ya Wenger, yalikuwa hivi: “Kile ndiyo kipindi tulikuwa na urafiki mkubwa na waandishi, pia nilijifunza kumbe upepo wa vyombo vya habari hutengenezwa na wanaoripotiwa. Kila upande ulizungumzia uzuri wa rekodi na mwisho nikajua kumbe waandishi na vyombo vyao walikuwa na presha kubwa kuliko mimi na wachezaji wangu, kwani walitaka kujua kila mwisho wa mechi ya Arsenal.”
Waandishi huripoti jambo na kutaka kulijua linakwenda vipi kwa lengo la taarifa, lakini nyumbani hapa, mambo ni tofauti kidogo kwa kuwa viongozi wa klabu hasa kongwe kama Yanga na Simba au Azam FC na nyingine zinazochipukia, huona shida sana kukosolewa kila inapotokea wakakosolewa, wanachotaka ni kusifiwa na wakisifiwa sana, hulalama eti wamesifiwa sana.
Angalia Simba wanavyoona wanaonewa kuhusiana na suala la Kocha Dylan Kerr ambaye walimleta wao, waandishi wa habari hawakumjua kabla na wakafanya siri kubwa ili wamtangaze wao na mtandao wao, kweli walifanya hivyo.
Mwisho wao ndiyo walimpa malengo wanayotaka na mshahara watakaomlipa na mambo mengine. Pia wakaishi naye wao, lakini mwisho mambo hayakwenda vizuri.
Wakati anakuja nchini, baada ya kuwa wamemtangaza, viongozi na wadau wa karibu wa uongozi wa Simba waliona raha Kerr kuhojiwa afahamike na wanachama na mashabiki wa Simba wapate taarifa zake.
Wakati wanaanza kuingia kwenye mzozo, hawakutaka tena ahojiwe na huenda kila ambaye atamhoji ataonekana kama vile ni msaliti, ana nia mbaya na huchelewi kusikia “Umetumwa na Yanga”, jambo ambalo ni kichekesho kikubwa hasa kwa mtu mwenye uwezo wa kutafakari.
Sasa ni kipindi cha Jackson Mayanja, kocha kutoka nchi jirani ya Uganda, kocha ambaye ninaamini kama hatadharauliwa kwa ajili ya Uafrika au ujirani wake kwa kuwa tu anatokea Uganda, anaweza kuisaidia Simba tena sana.
Hapa nianze na kukumbusha kwanza, kwamba Mayanja ametafutwa na Simba, amepewa kazi na Simba na klabu hiyo ndiyo inaishi naye ikimhudumia kila kitu.
Huenda kitakuwa kipindi kizuri cha kuishi milele kwa viongozi wa Simba kama ilivyokuwa kwa Wenger, kama watamsaidia naye awasaidie kwa kusaidiana na wachezaji na Simba itoke ilipokwama kwenye tope zito na kuanza kupiga hatua hadi itakapofikia ile kasi ya zamani iliyoipa sifa ya kuitwa, Simba.
Haya yote, hayawezi kupatikana kama ndani ya Simba kutakuwa na watu wenye maslahi yao binafsi na si ya klabu. Kusiwe na viongozi ndani ya klabu wanaotaka sifa ya kuonekana wao ndiyo wamesaidia sana kuliko wenzao na badala yake, Simba ibaki kuwa moja kama ilivyo kauli mbiu yake ya “Nguvu Moja”.
Viongozi lazima wajue msimu wa 2003-04 ambao Arsenal ilifanya vema na Wenger akaona aliishi milele si kitu kipya kwa Simba. Iliwahi kufanya hivyo ikiwa chini ya Kocha Patrick Phiri na lazima kulikuwa na umoja, ushirikiano wa juu ulioongozwa na upendo.
Kwa sasa ndani ya Simba, upendo upo, lakini wa ujanja. Urafiki upo, lakini una mashaka, nia ipo lakini ya kujenga nafsi binafsi. Vizuri mkaanza kuondoa kibanzi kwenye macho yenu, kabla ya kutanguliza lawama kwingine halafu, Simba itarejea kuishi milele kama kipindi cha Phiri au Wenger walivyoishi “milele”.
0 COMMENTS:
Post a Comment