Na Saleh Ally
Yanga imefungwa kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu Bara msimu huu. Coastal Union imeiangusha kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, jana.
Bao la kwanza la Miraji Athumani, lilikuwa la mkwaju wa faulo na makosa yalikuwa ya kipa Deo Munishi ‘Dida’.
Mpira ule ulifika mikononi mwaka, halafu ukamponyoka na kuingia wavuni.
Pamoja na makosa ya Dida, ukiangalia video ya bao hilo, utagundua mambo haya mawili.
MOJA:
Dida kweli hakutulia, kelele zilimbabaisha lakini presha ya wachezaji wanne wa Coastal ambao wanauzunguka ukuta wa Yanga wakimfuata yeye kwa kasi kubwa, ilichangia kwa kiasi kikubwa kwake kubabaika.
Wakati anafuatwa na wachezaji hao wa Coastal wakisubiri akosee wauwahi mpira, wachezaji wote wa Yanga walibaki wamezubaa na hawakuwa na msaada kama angeutema mpira ule. Inaonyesha lazima, Coastal ndiyo walikuwa na nafasi ya kufunga kwa asilimia 90 tena.
Hapa Yanga ingeokoka tu kama Dida angeukamata kabisa mpira huo, huenda pia kutaka kufanya hivyo, kulichangia umtoke. Kupangua ungekuwa uamuzi sahihi, lakini angefanya hivyo, bado Coastal ndiyo waliokuwa na nafasi ya kufunga tena.
MBILI:
Coastal wanaonyesha walikuwa tayari kwa ushindi katika mechi hiyo, walipania hasa kuwaangusha Yanga na kuondoka kwenye kundi la timu zinazodharauliwa.
Utaona walivyokuwa wamepania, utaona wakati ikipigwa faulo walivyokwenda kasi kama nyuki wanaomshambulia adui aliyegusa mzinga wao.
Namna Yanga walivyobaki, huenda walikuwa wakiamini mpiga faulo mzuri hawezi kuwa Coastal. Au walimwamini sana Dida kwamba asingefanya makosa, na huenda walijiamini mno wakiona, wao hawafungiki!
0 COMMENTS:
Post a Comment