Na Saleh Ally
WATU tunapenda soka kwa kuwa ni mchezo ambao unaburudisha sana akili, ingawa kuna wakati hugeuka na kuwa “kitengeneza” mawazo yanayoumiza.
Unajua timu inaposhinda mfululizo, anayeishabikia anakuwa ni mwenye furaha kuu na kuamini hakuna kinachofanana na timu yake. Majigambo ya kishabiki, yanatawala pia maneno ya kejeli kwa wengine, ili mradi ni kukamilisha furaha tu.
Kama timu itapoteza, machungu yanakuwa juu na mhusika huona kila kitu hakiendi sawa. Huenda wakati wa shida unaweza kuwa ndiyo sehemu nzuri ufahamu au uvumilivu wa shabiki wa timu fulani.
Labda nikutolee mfano namna mashabiki wa Simba walivyoonyesha uvumilivu wa hali ya juu kabisa wakati kikosi chao kikiwa na uongozi mpya chini ya Kocha Patrick Phiri kilivyotoa sare sita mfululizo.
Simba ilikuwa ‘inachekesha’ kwa maana ya muonekano, lakini mashabiki wake wengi waliendelea kuiunga mkono bila kujali baadhi yao walikuwa wamekata tamaa.
Msimu huu, katika timu tatu kubwa zinazowania zaidi ubingwa yaani Yanga, Simba na Azam FC, Simba ndiyo walikuwa wa kwanza kupoteza mechi mbili na kuwaacha Yanga na Azam FC wakicheza bila ya kupoteza mechi moja hadi wanafikisha mechi ya 15.
Bado mashabiki wa Simba waliendelea kuiunga mkono timu yao. Ikafikia uongozi ukamtimua Kocha Dylan Kerr, mashabiki hawakufurahia lakini mwisho wakabaki kuwa pamoja na timu yao hadi alipoajiriwa Jackson Mayanja ambaye anaonekana kuleta mabadiliko.
Katika mechi mbili zilizopita, Yanga wametoka sare moja na kufungwa moja. Maana yake wamedondosha pointi tano katika mechi hizo mbili na kuambulia moja tu walipotoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Prisons baada ya kuwa wamefungwa mabao 2-0 na Coastal Union.
Baada ya hapo, tayari mashabiki wa Yanga wameanza kusikika wakilalamika kupitia vyombo vya habari kwamba kocha hafai tena wanalia huenda inasababishwa na kuondoka kwa aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk Jonas Tiboroha!
Kulalamika kwa mashabiki wa Yanga ni sehemu ya sura sahihi kwamba asilimia kubwa ya wanaoupenda mpira ni wale wasiojua mwendo wa mchezo huo na kwa nini unapendwa na mashabiki wengi duniani.
Soka halina matokeo ya uhakika, jibu la usajili wa fedha nyingi haliwezi kuwa la moja kwa moja, au timu kuwa bingwa basi haiwezi kufungwa, bado haiwezi kuwa sahihi.
Yanga bado ipo kileleni ikiwa na pointi 40, Simba ya pili ikiwa na pointi 39, sawa na Azam FC ambayo ina viporo vya mechi mbili, lakini nani ana uhakika lazima Azam FC itashinda zote?
Nani ana uhakika Simba itaendelea kushinda tu au Azam FC itashinda tu na kuiporomosha Yanga? Nani ana uhakika hata Azam FC ikishinda viporo vyake, mbele haiwezi kupoteza?
Kuna maswali mengi ambayo yana majibu ambayo yanakwenda tofauti na mashabiki ambao wanatumia muda mwingi kulalamika kwenye vyombo vya habari, tena wakizungumza maneno ambayo yanaweza kuwakatisha tamaa wachezaji wao ambao wanapambana.
Kwa kifupi wanalazimisha kwenda mwendo ambao si sahihi, si wao na hautawezekana kwa kuwa katika soka, sare, kufungwa na kufunga vipo na si jambo geni hata kidogo!
Hakuna anayeona kwamba Yanga inacheza ikiwa na majeruhi wengi, ikiwakosa wachezaji kadhaa muhimu na inahitaji kubadilisha mambo kadhaa. Kulaumu tu kwa lengo la kujifurahisha, ni kuwachanganya zaidi wachezaji na kuondoa utulivu kikosi, hali itakayosababisha Yanga ipoteze zaidi.
Mashabiki wa Yanga lazima wajue, kikosi chao hakiundwi na malaika. Lazima kutakuwa na makosa, kutakuwa kuna kupanda na kushuka. Simba wamekuwa wavumilivu, walikuwa katika kundi la wasio na nafasi ya kutwaa ubingwa, lakini mashabiki wao wamewaunga mkono hadi sasa wameingia kwenye kundi la wenye nafasi ya kuwa mabingwa.
Kulaumu pekee, kwa maneno mengi ya kejeli kwa lengo la kuwaonyesha mashabiki au wanaokusikiliza kwamba unajua kusema, hakutasaidia kitu zaidi ya kusaidia kuwaangusha. Vizuri pia kujali sayansi ya ukweli lakini mwanzo lazima ungalie uhalisia na hali halisi ya unachokizungumza. Salamu kwenu.
Kweli huo ndio uanamichezo,yaani hata Saleh anawasihi wana Yanga kuwa watulivu.Big up kaka!
ReplyDelete