February 29, 2016



FRANCIS Cheka juzi akiwa ulingoni kwenye Viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar es Salaam, huenda ndiyo ulikuwa wakati pekee ambao Watanzania wanaomuunga mkono walikuwa na hofu kuu kuliko wakati mwingine wowote.

Cheka alikuwa anapambana kuwania ubingwa wa mabara dhidi ya Geard Ajetovic raia wa Serbia anayefanya kazi zake nchini Uingereza. Hakika lilikuwa ni pambano linalotisha kutazama hasa kama una moyo wa kizalendo.

Ajetovic aligeuka kuwa mwenyeji, alikuwa akimpiga Cheka kama mtoto mdogo. Alikuwa akimkimbiza ulingoni na kuchagua ampige wapi utafikiri mwenye bucha anavyochagua aikate upande upi nyama kabla ya kuipima kwenye mzani.

Kuna ile methali inayosema: “Kilio huanza na wafiwa ndiyo wengine wafuate.” Kwa kuwa Cheka ni rafiki yangu, mdogo wangu na Mtanzania mwenzangu mimi nimeamua kuanzisha kilio hiki na kutokukubali uzalendo wa “maboksi”, mvua ikinyesha unaloa.

Nilimuona Rais wa TPBO, Yassin Abdallah ‘Ustadhi’ akiwa ameshika kipaza sauti mara tu baada ya Cheka kutangazwa mshindi huku majaji wote wakimpa ushindi wa pointi 115-114, 115-114 na 116-111. Huu ni ushindi mkubwa unapozungumzia pointi majaji wote watatu wamempa ushindi Cheka.

Ustadhi alitumia muda mwingi akisema maneno ya kipuuzi kabisa. “Sisi siyo kichwa cha mwendawazimu kama wenzenu huko.” Hapa alikuwa akiwaponda watu wa soka kwamba wanafungwa tu.

Katika hali ya kawaida anakuwa ni mtu asiyejua maana ya mchezo wa timu na mchezo wa mmojammoja. Sijui kama aliwahi kuona kuna pasi ndani ya ngumi? Lakini hajui tofauti ya michezo hiyo na hajui hadhi yake na maneno yasiyo na maana.

Lakini hawezi pia kutambua namna Watanzania walivyoona kwa macho yao Cheka akidhalilishwa na baadaye akashinda. Kweli majaji wote wamempa ushindi, basi ni jambo la kujivunia kwa kuwa Watanzania wote tulitaka ashinde lakini kwa mara nyingine niendelee kuwa mkweli, si kwa ushindi ule.

Cheka amekuwa rafiki yangu kabla hajajuana na Ustadhi. Ningeweza kumpigia simu nikamueleza, lakini siwezi kuzungumza naye pembeni wakati alichokifanya kimetokea hadharani na Watanzania wote wameona kwamba alipigana na hakuwa katika kiwango sahihi.

Cheka alikuwa mwoga, hakuwa akijiamini, hakuwa na stamina, ngumi zake hazikuwa na nguvu na pumzi kama ilivyo kawaida yake haikuwa ya kutosha.

Siku chache kabla ya pambano lake, nilikutana na mtu akanieleza kwamba Cheka amekuwa akionekana katika sehemu za starehe, jambo aliloona si sahihi. Sikutaka kumwamini, hata sasa sitaki kumwamini kwa kuwa sijazungumza na Cheka kuhusiana na hili lakini ninaingia hofu katika hili.

Lazima Watanzania tuwe wakweli, wapenda haki na tunaokubali kukosolewa inapotokea kuna ukweli. Mimi ule ushindi wa Cheka sioni kama ni fahari ya Watanzania hata kama kweli mabondia wetu wamekuwa wakionewa nje.

Pamoja na wengine kuonewa, lakini haki imetendeka kwa wengi. Kumbuka Rashid Matumla ‘Snake Boy’ wakati huo, alitwaa ubingwa wa dunia nchini Afrika Kusini. Kabla yake, Magoma Shabani alibeba ubingwa wa Dunia wa WBO nchini Italia.

Haki ipo, basi na sisi lazima tulikubali hilo. Pia nimweleze Cheka bila ya kupindisha kwamba alikutana na bondia mzuri, lakini yeye alikuwa katika kiwango duni kuliko mapambano yote aliyowahi kucheza, ndiyo maana akawa anapigwa kama “punching bag”.

Tangu Cheka anapigana ngumi za ridhaa, nikimsindikiza hadi ulingoni, sikuwahi kuona akishindwa kukwepa ngumi, akishindwa kupiga ngumi na anakwenda kwa kuficha kichwa kwenye kamba.

Cheka anajua yeye ni fahari ya Watanzania. Asije akaisha kabisa kwa kupakwa sifa kwa mgongo wa chupa kupitia watu kama akina Ustadhi ambao hawawezi kupima ukweli ulio zaidi ya wazi.


Lazima Cheka arejee katika nidhamu yake ya awali ili aendelee kupambana akiwa katika kiwango bora. Kiwango chake dhidi ya Ajetovic kilikuwa kibovu, kisicho na mbinu na kulindwa na uvumilivu tu. Cheka anaweza kurejea, lakini bila ya kuamini alikosea na hakuwa vizuri juzi, atapotea kabisa.

1 COMMENTS:

  1. Saleh umesema kweli yote kabisa,sina cha kuongeza.
    Acheni kuhangaika na kufikiria jinsi ya kupata pesa kwa njia haramu,wewe copy & paste link ifuatayo baadae jisajili na kuanza kupiga mahela ukiwa na mtandao wako tuu.Huhitaji kutoa dhamana ya kitu chochote zaidi ya kuwatumia uwapendao hiyo link nao wafaidike.Link yenyewe ni:-http://InvitenShare.com/?ref=65321

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic