Pamoja na kudondosha pointi tano kati ya sita kwenye mechi dhidi ya Coastal Union na Prisons, mabingwa wa Kagame, Azam wamesema bado uhakika wa kuchukua ubingwa wa ligi kuu msimu huu upo palepale, lakini wakaitaja Simba kuwa nao wana nafasi kubwa ya kufanya hivyo.
Kichapo cha bao 1-0 mbele ya Coastal na suluhu dhidi ya Prisons wiki iliyopita, iliifanya Azam kubaki nafasi ya pili na pointi 46, sawa na Yanga walio kileleni, huku Simba ikishika nafasi ya tatu kwa pointi moja nyuma yao, lakini Wekundu wakiwa na mchezo mmoja mbele.
Kocha Msaidizi wa Azam FC, Denis Kitambi, amesema mpaka sasa hakuna timu inayoweza kujinadi kuwa ni bingwa na anaamini mmoja kati yao, Yanga na Simba ndiye mwenye nafasi ya kulibeba taji hilo, linalomilikiwa na Yanga kwa sasa.
Kocha huyo wa zamani wa Ndanda alisema awali Simba haikuwa akilini mwao kama mpinzani katika vita hii, wakiamini wapinzani wao wakuu wangekuwa Yanga lakini ghafla Simba wameingia kwenye rada hizo.
“Awali tuliamini wapinzani wetu ni Yanga kwenye vita hii, lakini Simba nao kwa sasa wanaonyesha wapo kwenye vita hiyo, hata kama walipoteza mbele ya watani wao, Yanga.
Kwa hiyo mpaka sasa picha ya ubingwa bado haijapatikana kati ya timu zote tatu lakini ukweli Simba nao wana nafasi kubwa ya kuweza kuuchukua,” alisema Kitambi.
Yanga watakutana na Azam Jumamosi ijayo katika mchezo ambao unaweza kutoa taswira kamili ya nani bingwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment