February 5, 2016


JKT RUVU

Na Saleh Ally
UKITAZAMA kwa asilimia kubwa sasa wadau wengi wa soka wameelekeza macho na masikio yao katika vikosi vitatu, kwamba nani kati yao atakuwa bingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Yanga, Simba au Azam FC, kati ya hizo timu gani inaweza kuibuka na kuchukua taji hilo ambalo kwa sasa limehifadhiwa kwenye kabati za ofisi ya katibu mkuu pale makao makuu ya Yanga, mitaa ya Jangwani na Twiga.

Mabingwa hao watetezi na Azam FC ndiyo walikuwa na nafasi zaidi wiki mbili zilizopita, lakini baada ya Simba kubadili kocha, kumng’oa Mwingereza Dylan Kerr na kumuachia mikoba Mganda, Jackson Mayanja, mambo yamebadilika.

Simba sasa ni kati ya wanaowania ubingwa. Ingawa wakati presha hiyo ya vigogo ikiendelea, angalia zaidi ya nusu ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara zina presha ya kuepuka kuteremka daraja.

Baada ya Yanga, Simba na Azam FC, hadi sasa huku timu nyingine zikiwa zimecheza mechi 15 hadi 17, ni Mtibwa Sugar, Mwadui, Stand na Prisons zinazoonekana ziko katika mikono salama kama zitaendelea na mwendo huo.
NDANDA FC

Nyingine tisa ziko kwenye presha ya kuteremka daraja na lazima zipigane vilivyo na kucheza karata zake vizuri kuepuka hilo.

Timu tisa zilizo roho mkononi ni Toto Africans yenye pointi 18, Mgambo (17), Kagera Sugar (15) na Mbeya City (14).

Nyingine ni Ndanda FC, Coastal Union, JKT Ruvu, Majimaji, hizi kila moja ina pointi 13 huku African Sports iliyo mkiani ikiwa na pointi 12.

Hakuna tofauti ya kimsingi kati ya African Sports na timu sita ambazo ni Majimaji, JKT, Coastal, Ndanda, Mbeya City hata Kagera Sugar. Kati ya hizo, ikiteleza mechi moja na Wanakimanumanu wakashinda moja, maana yake inawafikia au kuwapita.

Hii inafanya timu nyingi zaidi ya nusu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara kuwa katika presha kubwa ya kuepuka kuteremka daraja.

Ndani ya timu zinazoepuka kuteremka daraja, kama utaenda kwenye historia ya mpira wa Tanzania unakuta kuna timu nne zenye rekodi ya ukongwe ambazo ni African Sports, Coastal Union, Majimaji na Toto.

Kwa maana ya timu zilizochipukia hivi karibuni na kuwa tishio, Kagera na Mbeya City nazo zinaingia katika mkumbo huo wa presha na zinahitajika kuepuka kuwa roho mkononi ni kucheza karata zao kwa mpangilio mzuri kwelikweli.

TOTO AFRICAN
Presha inaweza kuwa juu zaidi kwa kuwa wingi au ukubwa wa wigo wa hiyo presha ya roho mkononi utakuwa mkubwa kwa kuwa ni timu nyingi zimeingia.

Itaongezeka zaidi kwa vile kama wigo ni mpana, timu hizo zitakutana mara nyingi. Mfano Toto, mechi zake nne zitakuwa dhidi ya wale walio katika wigo huo ambao ni Mbeya City, Kagera, Ndanda FC na JKT Ruvu.

Karata za kuwania ubingwa za Yanga, Simba na Azam FC zinaweza kuwa ngumu kweli ila karata za wanaowania kuepuka kuteremka daraja zinaweza kuwa za moto zaidi hata kuliko zile za ubingwa na hii ni kutokana na wigo mpana wa presha.

Upana wa wigo wa presha kuwa mkubwa, timu za chini kulingana pointi kwa asilimia kubwa au kuwa na tofauti ndogo, inaonyesha kwa misimu minne sasa, Ligi Kuu Bara msimu huu ndiyo imekuwa ngumu zaidi.

Huenda hili ni jibu la upatikanaji wa nafuu wa kifedha kwa kuwa angalau kuna fedha za wadhamini wa Ligi Kuu Bara kupitia runinga.

Ingawa zimeathirika kimapato kupitia getini, hasa kwa timu kubwa. Baadhi ya timu ndogo zimepata ahueni na kuongeza ushindani.

Ushindani huo unakwenda dhidi ya timu kubwa, lakini unazidi kuimarika dhidi yao, hivyo kutanua wigo wa presha ambao sasa unaonyesha hadi sasa, hata timu iliyo mkiani, hauwezi kusema iko katika hatari ya kuteremka daraja.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic