February 15, 2016

ANDY COLE NA SALEH ALLY


Na Saleh Ally
Mara nyingi sana ninachelewa kulala, ninawahi kuamka. Haya yamekuwa ni maisha yangu ya kila siku, hadi imefikia mara kadhaa madaktari wamekuwa wakinishawishi kulala kwa muda angalau wa saa tano na zaidi.

Wakati mwingine ninafuata masharti, lakini yote hayo sifanyi makusudi, inatokana na kutingwa na kazi nyingi. Pia ninapenda kuifanya iwe kazi nzuri na bora.

COLE AKIELEZEA UGONJWA WA FIGO UNAVYOMTESA
Wakati napitia mitandao kadhaa, nilikutana na stori ya mwanasoka maarufu wa England, Andy Cole. Kwamba sasa anapambana na kufeli kwa figo zake, tena zinazidi kupunguza uwezo wa kufanya kazi.

Hii ilinishitua sana, niliisoma kidogo tu stori hiyo kabla ya kuirudia mara nyingine leo. Nikaguswa zaidi na kuamua kushea nanyi wadau wangu kwa kuwa naona nilichowaza, kinatuhusu sote.

HUU NDIYO MWOKENANO WAKE WA SASA
Takribani mwaka mmoja nilifanya mahojiano ya ana kwa ana na Cole, huyu ni mshambuliaji aliyefunga mabao mengi zaidi, akiwa anashika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu England, tokea ianzishwe. Kinara ni Allan Shearer.

Cole amezichezea timu nyingi, lakini mafanikio makubwa yalikuwa Manchester United aliyoisaidia kutwaa makombe matano ya Ligi Kuu England pamoja na lile la Ligi ya Mabingwa.

Kama unazungumzia wafungaji, maana yake hakuna aliyewahi kufunga mabao mengi zaidi chini ya Ferguson kama yeye. Ni shujaa wa Manchester United.


Amecheza mechi 624 za Ligi Kuu England akiwa na Blackburn, Man United na Newcastle, amefunga mabao 271. Kaichezea England mechi 15. Huyu ni mtu fiti kabisa, hata kama atakaa muda mwingi bila kucheza soka, huwezi kutegemea aanze kusakamwa na magonjwa.


Cole aliyestaafu soka la ushindani mwaka 2008, sasa ana miaka 44, figo zake zinafanya kazi kwa asilimia 20 tu, hili si jambo la mzaha hata kidogo.

Wakati nazungumza naye nilimuuliza mambo mengi pamoja na afya kwa wale wanaocheza ligi kubwa kama ya England. Akasema mtu lazima awe imara hasa kiafya na kusisitiza yeye ataendelea kujilinda kwa kuwa afya yake ni njema zaidi.

Aliwahi kujua mapema ana matatizo ya figo, lakini juhudi zilifanyika kumfanya awe fiti na kweli akaendelea kuitumikia timu yake vizuri na kuisaidia kwa kiasi kikubwa.
Lakini leo anaonekana ni mtu aliyenenepa sana, hii ni kutokana na ugonjwa huo hatari wa figo unaomsumbua sana.

Nilianza kujiuliza hivi, Cole, aliyecheza ligi ngumu, leo tayari ni mgonjwa wa figo, anaonekana kihali, hayuko vizuri.

Muonekano wake, hakika unatia hofu, unaonyesha ni mtu mwenye unene usio na afya sahihi. Takribani mwaka tu na ushee tokea nionane naye.

Angalia, shujaa wa England, shujaa wa Manchester United klabu kubwa. Mtu mwenye fedha zake, tena alikuwa mchezaji imara kabisa.

Lakini naye analalamika kuumwa, tena ugonjwa wa figo ambao huenda ungewasumbua watu masikini kama Saleh Ally au Watanzania wengine.


Huenda nilikuwa nina mazazo yasiyo sahihi, nikaanza kurudi nyuma na kumsikitikia Cole kwa kuwa nilimuona mtu mstaarabu, msikivu na mwenye msaada kikazi nilipokutana naye.
Staa mkubwa, lakini hana maringo. Mwenye kutoa ushirikiano na hata Airtel waliomleta, walimsifia kwa kuwa mwenye tabia ya upendo.

Leo anaumwa, kuumwa kwake kumenigusa kwa huruma ya kibinadamu. Lakini pia nimerejea na kuamini, kuumwa ni kwa yoyote bila kujali alikuwa fiti sana, alicheza ligi ngumu sana, yoyote anaweza kuingia kwenye matatizo wakati wowote.

Mungu ndiye kiongozi na anajua kesho ya kila mmoja wetu. Vizuri kumuomba na kumshukuru, vizuri kumuamini na kumuabudu kwa dhati.

Kutoka moyoni, namwombea Cole apate nafuu na ikiwezekana arejee katika hali nzuri kwa kuwa kwa Mwenyezi Mungu, hakuna kinachoshindikana.











1 COMMENTS:

  1. Saleh, nami nimeguswa na makala yako. Uko sahihi kabisa kwa sababu maisha yetu yako mikononi mwa Mungu. Nami nina mfano wa ndugu yangu mmoja ambaye ni mtu wa mazoezi sana - karateka - na alikuwa fiti sana lakini cha ajabu akaja kukumbwa na ugonjwa mbaya wa kiharusi, hata tunajiuliza kimepita wapi wakati ni mtu wsa mazoezi sana. Nimependa sana maneno yako ya mwisho kwenye makala yako. Naomba nimalizie kwa kunukuu maneno hayo na yawe dira yetu kila iitwapo leo tunapoendelea kumtegemea Mungu maishani mwetu: "Lakini pia nimerejea na kuamini, kuumwa ni kwa yoyote bila kujali alikuwa fiti sana, alicheza ligi ngumu sana, yoyote anaweza kuingia kwenye matatizo wakati wowote. "Mungu ndiye kiongozi na anajua kesho ya kila mmoja wetu. Vizuri kumuomba na kumshukuru, vizuri kumuamini na kumuabudu kwa dhati." Sote tunamuombea Andy Cole apone na apate nguvu ili aendelee na maisha yake.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic