Yanga itamrudisha Rwanda kiungo wake Haruna Niyonzima kwenda kucheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya APR, hii ni baada ya juzi kuitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0 juzi.
Yanga ilishinda bao 1-0 likifungwa na Donald Ngoma ugenini, kabla ya juzi mabao ya Amissi Tambwe na Thaban Kamusoko kuihakikishia nafasi ya raundi ya kwanza.
APR, ambao walimuachia Niyonzima kutua Jangwani mwaka 2011 baada ya kuitumikia misimu minne, yenyewe ilifuzu kwa jumla ya mabao 4-2 mbele ya Waswaziland, Mbanane Swallow.
Kwa mujibu wa ratiba, Yanga itaanzia ugenini Machi 12, mwaka huu kabla ya kurudiana Machi 19 jijini Dar. Mshindi kati yao, kuna uwezekano mkubwa akakutana na wababe wa Wamisri, Al Ahly ambayo ilikuwa ikisubiri mshindi kati ya Libolo ya Angola na Micomeseng ya Guinea ya Ikweta.
Mbali na Yanga, baadhi ya timu zilizofanikiwa kuvuka hatua hiyo juzi Jumamosi ni Ferroviario Maputo ya Msumbiji iliyokuwa ikisubiri mshindi kati AS Vita ya DR Congo na Mafunzo ambao ni wawakilishi wengine wa Tanzania. Mchezo wa kwanza Mafunzo ilifungwa mabao 3-0 nyumbani.
Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini sasa watakutana na Leopard ya Congo. Timu nyingine zilizofuzu ni Warri ya Nigeria, Al-Merreikh ya Sudan, Tripoli ya Libya na Al-Hilal ya Sudan huku St. Georges ya Ethiopia wao watachuana vikali na mabingwa watetezi, TP Mazembe ya DR Congo.
Timu nyingine zilitarajiwa kupatikana jana katika michezo ya marudiano.
0 COMMENTS:
Post a Comment