March 9, 2016


Yanga kama wameshtukia vile, hiyo ni baada ya kumbadilishia hospitali nahodha na beki wao wa kati, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwa ajili ya matibabu.

Awali, beki huyo alikuwa nje ya uwanja kwa muda wa wiki tatu kabla ya kurejea uwanjani hivi karibuni na kushauriwa kusimama mazoezi ili aendelee na matibabu ya kifundo cha mguu ‘enka’.

Beki huyo, alipata majeraha hayo kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Etoile du Sahel katika mchezo wake wa pili kabla ya kujitonesha akiwa anaitumikia Taifa Stars.

Cannavaro alisema uongozi wa timu yake umembadilishia hospitali kutoka Muhimbili ya jijini Dar es Salam iliyomshauri wamfanyie upasuaji kwenye jeraha hilo.

Cannavaro alisema, uongozi wa timu hiyo umemhamishia kwenye moja ya hospitali kubwa iliyopo Upanga Dar es Salaam inayohusika na masuala ya viungo pekee.

Aliongeza kuwa, madaktari wa hospitali hiyo tayari wamemuandalia ratiba maalum ya kuhudhuria kliniki kila baada ya siku tatu kwa ajili ya matibabu ili apone haraka kuhakikisha anarejea uwanjani.

“Kama unavyojua tangu matibabu yangu ya awali nilikuwa ninafanya kwenye hospitali ya Muhimbili ambayo hivi karibuni madaktari walinishauri nifanyiwe upasuaji.

“Lakini baada ya majibu hayo, viongozi wa Yanga wakaona wanibadilishie hospitali kwa ajili ya matibabu zaidi, na baada ya kufanyiwa uchunguzi ikabainika kuwa ninaweza kupona bila ya upasuaji wowote.

“Hivyo hivi sasa nimeanza matibabu kwenye hospitali hii mpya na tayari nimepangiwa ratiba ya kuhudhuria kliniki kila baada ya siku tatu kwa kuanzia keshokutwa (kesho) Alhamisi,” alisema Cannavaro.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic