Baada ya kuonekana safu ya ushambuliaji wa Yanga inayoundwa na Simon Msuva, Mrundi Amissi Tambwe na Mzimbabwe Donald Ngoma kuwa hatari na kuitisha APR, lakini ni kama wamejipalia makaa kutokana ubora wa mabeki wa wapinzani wao.
Yanga inayotarajia kucheza na APR Jumamosi ya wiki hii katika mchezo wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa kwenye Uwanja wa Amahoro jijini Kigali, Rwanda.
Licha ya APR kuingia mkataba kimyakimya na kocha raia wa Tunisia, Nizar Khanfi, ili kuimarisha kikosi hicho lakini gumzo kubwa limebaki kwa washambuliaji hao walipachikwa jina la MTN ambao ni Msuva, Tambwe na Ngoma.
Kocha wa timu ya Taifa ya Rwanda ‘Amavubi’ Johnny McKinstry, raia wa Ireland ambaye alikuwepo nchini wikiendi iliyopita kushuhudia mchezo kati ya Azam FC na Yanga, alisema licha ya Yanga kuwa na safu nzuri ya ushambuliaji lakini itakuwa katika wakati mgumu kupambana na mabeki wa kati wa APR ambao wamekuwa wakicheza kwa uelewano mzuri.
“Unajua mchezo utakuwa mgumu sana kwa sababu Yanga inajivunia pacha yake ya MTN ambayo ipo vizuri sana katika kushambulia lakini bado ina wakati mgumu kwa safu ya ulinzi ya APR inayongozwa na Albert Ngabo na Abdul Rwatubyaye, siyo watu wakufanya makosa ya mara kwa mara.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kuiona Yanga ikicheza na wana timu mzuri kutokana na jinsi wanavyocheza maana hata katika mchezo huo naamini lazima Haruna Niyozima wanaweza kumtumia katikati kwa sababu ya uzoefu wake na anaifahamu vizuri APR ingawa naye atapata upinzani kutoka kwa viungo kama APR kwani haitokuwa kazi rahisi,” alisema McKinstry.
0 COMMENTS:
Post a Comment