March 30, 2016

JAVU (KULIA) AKIWA YANGA

Mshambuliaji Hussein Javu hayupo kwenye kikosi cha Mtibwa Sugar kwa takriban muda wa wiki tatu sasa akisumbuliwa na maumivu ya tumbo ambayo mpaka sasa haijajulikana nini hasa kinamsumbua.

Javu aliyerejea Mtibwa mwanzoni mwa msimu huu akitokea Yanga SC, ameshindwa kuitumikia timu hiyo kutokana na maumivu hayo tangu walipotoka kushiriki kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, Zanzibar miezi mitatu na wiki mbili zilizopita.

Javu amesema tumbo hilo limekuwa likimsumbua mara kwa mara lakini muda mwingine linapoa na akirejea kazini linaanza kumsumbua tena mpaka alipoamua kukaa kando kushughulikia tatizo hilo wiki chache zilizopita.
“Nimepima kila kitu lakini hakuna tatizo na nimetoka kwenye hospitali za Dar es Salaam hivi karibuni tu lakini nao hawakuona tatizo, nimeamua kutumia dawa za asili, hizi za mitishamba ya kawaida wanazijua wazee wa zamani ambazo angalau sasa zimenipa mabadiliko.
“Lakini hapo kabla nimeteseka sana, nimeumwa sana kwa kweli, nasikia hamu ya mpira na keshokutwa (leo Jumatano) natarajia nikaanze mazoezi kidogokidogo ingawa wasiwasi wangu lisije kuanza tena, maana hata siku za nyuma nilikuwa napata nafuu, nikirejea mazoezini linaanza tena, sasa sijui itakuwaje, naomba Mungu anisaidie,” alisema Javu.

Alipotafutwa Kocha wa Mtibwa, Mecky Maxime, kuhusiana na hilo alisema: “Javu anaumwa, kwenye timu hayupo muda kidogo kwa ajili ya matibabu zaidi. Lakini nimewasiliana naye amesema anaweza kuja kuanza mazoezi Jumatano (leo) ila kikubwa ni tumbo ndiyo linamsumbua na haijajulikana hasa ni kitu gani.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV