Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, ametamka kuwa ameandaa mbinu za kuhakikisha kikosi chake kinafanikiwa kutinga katika hatua ya makundi kwa kuwaondosha Waarabu Al Ahly ambapo amepanga kumaliza kila kitu kwenye mchezo wa kwanza baina ya timu hizo zitakapokutana nchini.
Pluijm amesema kuwa mbinu pekee ambayo itaitumia kuwaondosha Waarabu hao ni kuhakikisha kikosi chake kinaibuka na ushindi kwenye mchezo wa hapa kwa kushambulia kwa muda mwingi kutokana na staili za uchezaji za timu za Kiarabu ambazo mara nyingi zinasaka sare kabla ya kwenda kushinda kwao lakini pia kufanya kila jitihada kuwabana wapinzani wao wasiweze kupata bao lolote kwenye mchezo huo.
Yanga itashuka dimbani dhidi ya Al Ahly Aprili 9, mwaka huu kukumbana na Waarabu hao katika mechi itakayopigwa Uwanja wa Taifa, Dar ambapo wataingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kutupwa nje na timu hiyo kwenye kombe hilo kwa mikwaju ya penalti mwaka 2014, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 kwenye michezo yote miwili.
Pluijm ambaye ni kocha wa zamani wa Berekum Chelsea ya Ghana, amesema kuwa ni lazima wamalize pambano hilo kwa kushinda katika uwanja wa nyumbani tena wa mabao mengi zaidi kwa ajili ya kujisafishia njia ya kusonga mbele zaidi kwa kuwapa wapinzani wao shida ya kuweza kurejesha mabao hayo kwenye mechi ya marudiano.
“Ni lazima tumalize kila kitu kwenye mechi yetu dhidi ya Al Ahly tukiwa hapa nyumbani kwa kuweza kuibuka na ushindi, tena ule wa mabao mengi na siyo wa bao 1-0 kwani wapinzani wetu mara nyingi wakiwa ugenini wanakuwa na tabia ya kusaka sare au kufungwa kwa idadi ndogo ya mabao kabla ya kwenda kuwaadhibu wanapokuwa kwao.
"Lakini pia tunatakiwa tujilinde kwa hali ya juu kwa kutoruhusu nyavu zetu kutikiswa.
“Kwani kama tukiweza kushinda mechi ya hapa nyumbani, basi mzigo hautakuwa mkubwa pia tukirudiana nao lakini pia tutawafanya wao wacheze kwa presha ya kuweza kurudisha mabao.
"Hivyo watafunguka na hiyo inaweza kuwa sababu nyingine ya sisi kupata mabao kwenye mchezo huo kwani watakuwa wanashambulia sana bila kujilinda,” alisema Pluijm.
0 COMMENTS:
Post a Comment