March 4, 2016



Na Saleh Ally
SAKATA la beki Hassan Isihaka na uongozi wa Simba ni kati ya mambo gumzo kubwa katika medani ya soka lakini mimi limenipa funzo kubwa sana, nitakueleza.

Kwanza nikukumbushe kwamba Isihaka alipangwa na Kocha wa Simba, Jackson Mayanja acheze mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Singida United. Uongozi wa Simba ukaeleza, kinda huyo alitoa maneno yasiyo ya kiungwana. Ukatangaza kumsimamisha kwa muda usiojulikana.

Wakati umetangaza, muda mchache baadaye, mshambuliaji wa Simba, Hamis Friday Kiiza, akatupia ujumbe kupitia Mtandao wa Kijamii wa Instagram akisema Isihaka alikuwa anachafuliwa, tena akimalizia kwa kusema Mungu yupo!

Siku iliyofuata, Isihaka akaomba radhi kwa kitendo chake cha kumtolea Mayanja maneno yasiyo ya kiungwana. Hadi jana mchana, uongozi wa Simba haukuwa umesema kama umepokea msamaha huo na uamuzi ni upi. Ukiniambia mimi nitaushauri kumsamehe kwa kuwa ameona kosa mapema na baada ya hapo, nguvu iwe katika mechi zao zijazo kwa kuwa ndiyo kilichowakutanisha.

Lakini sitakubali lipite bila ya kumzungumzia Kiiza, mshambuliaji anayeongoza kwa kufunga mabao katika kikosi cha Simba na Ligi Kuu Bara kwa jumla. Ana mabao 16, jambo jema na la kujivunia.

Kwa wachezaji anaocheza nao Simba, yeye ni kati ya wale wanaoweza kujiita wazoefu zaidi kama si wakongwe ila anaonekana kutokuwa na busara na akiendelea hivyo atafeli.


Ninajua mtazamo wa mashabiki huenda wakawa wanamtazama Kiiza kwa faida ya mabao yake pekee, lakini wakasahau wenye vipaji kibao wamefeli kwa kuwa walishindwa kuitanguliza nidhamu kuwa muongozo katika maisha yao. Nitakueleza kwa nini nikianza na hilo la Kiiza.

Tarehe 29 iliyokuwa siku ya mwisho ya Februari, saa 11 jioni, Msemaji wa Simba, Haji Manara, alitoa taarifa kueleza kusimamishwa kwa Isihaka baada ya kumtolea kocha wake maneno yasiyo na staha. Taarifa hiyo ikaanza kutembea kwa kasi mitandaoni.

Kuanzia saa tatu usiku, siku hiyohiyo, mitandaoni maneno aliyoandika Kiiza katika akaunti yake ya Instagram, yakaanza kuzagaa akimtetea Isihaka na kusema kwamba anampenda sana, ni mtu mwenye nidhamu, hana matatizo, huku akisisitiza mambo ya kuharibu jina la mtu si vizuri.

Bila ubishi ilionekana wazi kwamba hakufurahishwa na adhabu aliyopewa Isihaka, jioni ya siku hiyo. Siku iliyofuata, Isihaka alikubali kosa lake na kuanza kusikika kwenye vyombo vya habari akiomba radhi, naamini lilikuwa jambo zuri.


Nilianza kutafakari kuhusiana na Kiiza, ambaye alionyesha kupinga taarifa iliyotolewa na uongozi. Alionyesha kwamba Isihaka hakukosea kwa kusema ni mtu mwenye nidhamu sana katika kipindi ambacho ametoka kuonyesha utovu wa nidhamu kwa kocha wake. Nilisikia uongozi ulimtaka kuomba radhi na kumsisitiza kuandika tena kwenye mtandao kuhusiana na alichokosea.

Kiiza aliibuka na kuandika kujaribu kurekebisha alichokuwa amekisema kuhusiana na Isihaka na namna ilivyoonekana kama anapingana na uongozi.

Ajabu alichokiandika kilikuwa kitu cha uongo, kinachoshangaza na hautegemei mchezaji anayeweza kufunga mabao mazuri anaweza kushindwa kuwa muungwana na kuona kosa, akalikubali na kuomba msamaha badala yake analiangushia kwa wengine.


Huenda sasa aliona aibu baada ya Isihaka kukubali kuomba radhi, pia uongozi wa Simba kuonyesha kuchukizwa. Badala ya yeye kuomba radhi, akaiangushia kesi kwa magazeti, jambo ambalo ni uongo mtupu.

Alianzia kwamba, anakubali Isihaka alifanya kosa, anasema eti alijisikia maumivu baada ya kuona magazeti yameandika eti alimtolea matusi kocha kwa kuwa yanataka kuuza!

Kwangu hiki kilikuwa kichekesho cha wiki! Simba ilitoa taarifa yake Jumatatu saa 11 jioni, usiku huohuo taarifa zikaanza kusambaa mtandaoni Kiiza akidai Isihaka anachafuliwa. Sasa kuna gazeti lilitoka usiku huo? Au kuna gazeti lilitoka kati ya saa 11 jioni na saa tatu usiku? Hovyo kabisa. Huenda Kiiza anadhani ni ‘smart’ sana kuliko kila Mtanzania aliye hapa nchini, kitu ambacho anajidanganya kabisa.

Angekuwa muungwana, hakupaswa kudanganya, badala yake angeomba radhi kwa upuuzi alioufanya. Isihaka alikosea, Simba ndiyo ilitoa taarifa naye alipaswa kukaa na Isihaka kama rafiki au mdogo wake ili kumrekebisha.

Lakini si kumuonyesha mapenzi ya macho ya samaki, mzima yako wazi, kafa yako wazi pia na hayajawahi kufumba! Kufanya hivyo haitakuwa kumuonyesha mapenzi, badala yake ni kuendelea kumshawishi aendelee kufanya makosa.

Alipoona amekosea, huenda angekuwa kama alivyofanya Isihaka. Angeomba radhi badala ya kuyaangushia magazeti eti yanataka kuuza. Wakati anaandika maneno yake ya hovyo mtandaoni hakuna gazeti lililokuwa limeandika stori hiyo ya Isihaka. Muungwana hukubali kosa badala ya kutenda kosa juu ya kosa sababu ya kukwepa kosa.

Hata Lionel Messi asingekuwa na nidhamu asingefika hapo. Nidhamu ndiyo mwongozo wa maisha ya kila mtu. Kiiza anapaswa kuiheshimu Simba hata kama inamtegemea. Hakuna mchezaji anayeweza kuwa mkubwa kuliko Simba. Kiiza acha siasa si upande wako, pia kumbuka, bila nidhamu utaishia njiani. 



2 COMMENTS:

  1. Haaaa! Huyu nae.....

    ReplyDelete
  2. MESSI ANGEKUWA NA NIDHAMU ASINGEPELEKWA MAHAKAMANI KWA KUKWEPA KODI,TAFUTENI KUMBUKUMBU SAHIHI!VIONGOZI WA SIMBA HAWAJUHI MPIRA ZAIDI YA FITINA ZA KIJINGA TUU

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic